"Yeye ni kama baba ambaye walitamani" Esther Musila amsifia Guardian Angel kufuatia uhusiano mzuri na wanawe

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wa watatu alisema Guardian Angel sio tu baba wa kambo wa wanawe bali pia rafiki wao mkubwa, mshauri na msukumo mkubwa katika maisha yao.

•Alisema mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili anawapenda watoto wake sana na kuwawajibikia kama ndiye baba mzazi.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Esther Musila amemlimbikizia mpenzi wake Peter Omwaka almaarufu kama Guardian Angel sifa kochokocho kwa mazuri aliyomtendea maishani.

Alipokuwa anazungumza katika hafla ya kuzindua albamu mpya ya Guardian Angel, Bi Musila alifichua mwanamuziki huyo ana uhusiano mzuri wa karibu na watoto wake ambao tayari ni watu wazima.

Mama huyo wa watoto wa watatu alisema Guardian Angel sio tu baba wa kambo wa wanawe bali pia rafiki wao mkubwa, mshauri na msukumo mkubwa katika maisha yao.

"Guardian ni rafiki. Ameweza kuwasaidia. Labda yeye  ndiye baba walitamani kuwa naye. Hata kama wako na baba mzazi. Wao ni marafiki. Wakati mwingine wanaenda nyuma yangu na kuandika wanataka pesa" Esther alisema.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 51 alisema uhusiano mzuri ambao mpenzi wake Guardian Angel ameweza kujenga na wanawe umempatia msukumo wa kumpenda na kumsherehekea zaidi.

Alisema mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili anawapenda watoto wake sana na kuwawajibikia kama ndiye baba mzazi.

" Anawapenda kama watoto wake. Huwa anawaongelesha. Kuna mambo ambayo binti yangu hawezi niambia lakini huwa anamwambia yeye. Yeye ni kama ndugu, huwa wanaitana G" Esther alisema.

Bi Musila pia aliweka wazi kuwa mara ya kwanza walipojuana na mwanamuziki huyo hakudhani wangewahi kuwa wapenzi ila baada ya kujuana kwa kipindi wakaanza kuchumbiana.