"Buda unachoma!" O.J amkemea 'mjomba' wake Omosh kwa kukosa kutosheka

Muhtasari

•O.J alisema hana chuki yoyote kwa mwigizaji huyo ambaye aliigiza kama mjomba wake katika kipindi cha Tahidi High ila akadai amechoshwa  sana na tabia zake.

•Pia amewaonya Wakenya dhidi ya kuanguka kwenye mtego wa kumchangia Omosh tena huku akieleza kuwa yeye sio mwajibikaji.

Omosh na OJ
Omosh na OJ
Image: HISANI

Mwigizaji  Dennis Mugo almaarufu kama O.J amemkosoa sana aliyekuwa mwigizaji mwenzake katika kipindi cha Tahidi High Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh.

Alipokuwa kwenye mahojiano na 'Glow up with Makena' hivi karibuni, O.J alikosoa kitendo cha Omosh cha kuomba msaada mara kwa mara hata baada ya Wakenya kujitolea sana kumsaidia alipoeleza masaibu yake mara ya kwanza.

O.J alisema hana chuki yoyote kwa mwigizaji huyo ambaye aliigiza kama mjomba wake katika kipindi cha Tahidi High ila akadai amechoshwa  sana na tabia zake.

"Buda unachoma! Omosh unachoma! Buda tutakusaidia mara ngapi wewe? Nimechoka na wewe! Nampenda lakini yeye ni mjinga. Huo ndio ujumbe wangu kwake" Alisema O.J.

Mwigizaji huyo ambaye kwa sasa anafanyia serikali ya kaunti ya Embu kazi pia amewaonya Wakenya dhidi ya kuanguka kwenye mtego wa kumchangia Omosh tena huku akieleza kuwa yeye sio mwajibikaji.

"Wakenya endeleeni kuchanga, ata nyinyi mnachoma. Badala ya mtu kujitokeza na kuambia Omosh kuna rehab, kuna kanisa na mambo kama hayo mnachanga mnamnunulia nyumba yenye anataka kuuza saa hii. Mimi siko hapo" Omosh alisema.

Omosh amekuwa akivuma sana kwa kipindi kirefu mwaka huu baada yake kujitokeza mara kadhaa akiomba Wakenya msaada huku akidai amefilisika.

Tayari amepokea msaada wa pesa, nyumba na vitu vingine ambavyo anadaiwa kutumia vibaya ili kukimu kiu chake cha pombe .

O.J alifichua kwamba pia yeye alikuwa mraibu wa pombe hapo awali ila kwa sasa anaweza kujithibiti kiwango anachobugia.