"Nilijiuliza kama mimi ni mwanaume kamili" Daddy Owen afunguka kuhusu aliyopitia baada ya ndoa yake kuvunjika

Muhtasari

•Owen amesema yaliyotokea yalimfanya ajiulize maswali mengi na afanye mambo mengi yasiyo ya maana almradi tu ajithibitishie kuwa angali mwanaume.

•Ameweka wazi kuwa hajashiriki tendo la ndoa na mwanamke yeyote katika kipindi hicho licha ya kuwa ndoa yake ilisambaratika.

•Mwanamuziki huyo amesema hana mipango ya kuchumbia mwanamke mwingine kwa sasa kwani hali yake ya kihisia yaweza weka mpenzi wake mwingine hatarini

Image: INSTAGRAM// DADDY OWEN

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu kama Daddy Owen amefunguka kuhusu mambo ambayo amekuwa akipitia tangu alipotengana na mkewe takriban mwaka mmoja uliopita kuhusiana na suala la udanganyifu kwa ndoa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo amesema jambo hilo lilimfungulia milango ya hisia tofauti ambazo zilimfanya apatwe na msongo wa mawazo.

Owen amesema yaliyotokea yalimfanya ajiulize maswali mengi na afanye mambo mengi yasiyo ya maana almradi tu ajithibitishie kuwa angali mwanaume.

Kwa mwaka mzima nimekuwa na hisia tofauti! Kuishi peke yangu kulifanya iwe ngumu zaidi! Kulifanya nijiulize maswali mengi! Kama mimi mwanaume wa kutosha? Je, mimi ni maskini au tajiri? Je, yote hayo ni ya lazima? Hali hiyo ilinifanya ninunue vitu vya bei ghali visivyo vya lazima ili tu kujithibitishia kwamba ninaweza! Hali hiyo ilinifanya nisafiri mbali na kulipa hotelini ili tu kuthibitisha kwamba ninaweza! Msongo wa mawazo ulinifanya nicheze na watu ili tu kudhihirisha kuwa bado ni mwanaume!!" Daddy Owen amesema.

Owen amesema hajivunii yale aliyofanya kwa wakati huo huku akieleza kuwa aliyafanya kwa kuwa alikuwa ameathirika vibaya kihisia.

Amedai kuwa alitubu dhambi alizofanya na kuwaomba msamaha wote ambao waliathiriwa na yale aliyokuwa anapitia.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa hajashiriki tendo la ndoa na mwanamke yeyote katika kipindi hicho licha ya kuwa ndoa yake ilisambaratika.

"Je, ninajivunia? HAPANA! Nilijisikia vibaya na nilitishika, chochote kuhusu mimi kutaniana au kitu chochote cha aina hiyo ni kwa sababu niliathirika  kihisia ... nilikuwa na mashaka juu yangu mwenyewe! Je, niliomba msamaha kwa watu wanaohusika? NDIYO! Je, nilitubu na kumwomba MUNGU msamaha? NDIYO! Nimevuka mpaka??Je, nilikula tunda? (Najua wengi wenu mnataka tu kujua sehemu hiyo..) HAPANA! Sikula tufaha lolote .. bado natumia android!. Je, mimi ni Mtakatifu? Je, mimi ni mtakatifu kuliko wewe? HAPANA KABISA! Ina maana nina nguvu? HAPANA! Naamini ninaongozwa na kulindwa tu na ROHO MTAKATIFU! Kwa kweli dhambi ingetaka kukuondoa lakini kadiri ninavyoomba na kukaa katika NENO ndivyo ROHO MTAKATIFU ​​anavyopigana vita vyangu" Amesema Daddy Owen.

Mwanamuziki huyo amesema hana mipango ya kuchumbia mwanamke mwingine kwa sasa kwani hali yake ya kihisia yaweza weka mpenzi wake mwingine hatarini.

"Je, unachumbiana? Unapanga kuchumbiana hivi karibuni? HAPANA! Kwa nini? ..Nadhani fujo kama hiyo ya kihemko huwafanya watu kubeba sana mioyoni mwao na hiyo ni hatari kwa mwenzi anayefuata ambaye anaweza kuwa hana hatia. Udhaifu wa Btw ndio nguvu yangu. Mimi si Mtakatifu bali ni mwanadamu.. si mtu tu.. bali ni MTU WA MUNGU! Je, unapanga kuivua pete yako?????" Amesema.

Hivi majuzi mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro na ambaye ni wakili wa mwanamuziki huyu alimshauri atafute mpenzi mwingine sasa.