Kando na Briana, wafahamu wanadada wengine ambao Harmonize amewahi kuchumbia

Muhtasari

•Hapo awali Harmonize amekuwa kwenye mahusiano na wanawake kadhaa ila hakuna ambayo yameweza kudumu.

Harmonize na Briana
Harmonize na Briana
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Hivi majuzi mwanamuziki Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ametambulisha mpenzi wake mpya  hadharani baada ya kukaa kipindi cha takriban nusu mwaka bila mchumba.

Staa huyo wa Bongo alimtangaza Briana kama malkia mpya kwenye ufalme wake huku akiahidi  kumpenda na kumlinda.

Siku za hivi karibuni Harmonize na mwanadada huyo anayeaminika kuwa na asili ya Australia wamekuwa wakionekana pamoja katika maeneo mbalimbali ya burudani nchini Marekani ambako Harmonize amekuwa kwa muda katika ziara ya kimuziki.

Hapo awali Harmonize amekuwa kwenye mahusiano na wanawake kadhaa ila hakuna ambayo yameweza kudumu.

Kando na Briana, kuna angalau wanawake wengine wanne ambao mwanamuziki huyo anajulikana kuchumbia:-

Jacqueline Wolper

Harmonize na Jacqueline Wolper
Harmonize na Jacqueline Wolper

Mwanamitindo na mwigizaji mashuhuri kutoka Tanzania Jacqueline Massawe ni mpenzi wa kwanza wa Harmonize ambaye anajulikana.

Wasanii hao wawili wa bongo walichumbiana kati ya mwaka wa 2016 na 2017 kabla ya mahusiano yao kufika kikomo katika hali tatanishi.

Walipotengana takriban miaka minne iliyopita, Wolper alimnyooshea Harmonize kidole cha lawama na kumshtumu kuwa mdanganyifu kwa ndoa.

Hata hivyo, mwaka uliopita Harmonize alijitokeza kupuuzilia mbali madai hayo huku akidai kuwa Wolper alikuwa na mazoea ya kutoka nje ya ndoa mara kwa mara.

Harmonize alisema Wolper hakuzingatia mipaka ya mahusiano na hata alimmezea mate aliyekuwa mwenzake katika Wasafi, Diamond Platnumz.

Sarah Michelloti

Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Image: HISANI

Wawili hao walichumbiana kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kutengana mwaka uliopita baada ya  Sarah kugundua kuwa Harmonize alikuwa amecheza karata nje ya ndoa na hata kupata mtoto na mwanadada mwingine.

Hivi majuzi Harmonize alifichua kuwa ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto.

Harmonize alisema kuzaliwa kwa mtoto huyo kuliibua mzozo mkubwa katika ndoa yao kwani walibishana kila siku kuhusu suala hilo. 

Alisema ilifikia wakati akaweka mapenzi yake kwa bintiye kabla ya yale aliyokuwa nayo kwa mkewe  na hapo ndipo wakatengana.

Kwa kipindi cha miaka minne ambacho walichumbiana wawili hao walionekana kupendana sana na kufaana.

Harmonize ameonekana aghalabu akiomba Muitaliano huyo msamaha kwa maumivu ambayo alimsababishia moyoni.

Shanteel (Baby mama)

Official Shanteel, kama anavyojitambulisha kwenye mtandao wa Instagram ni mwanadada ambaye Harmonize alijitosa kwenye mahusiano ya kipindi kifupi naye wakati Sarah alikuwa amefunga safari ya kuenda kwao.

Ingawa mahusiano yao hayakudumu sana wala kuzungumziwa sana, wawili hao waliweza kubarikiwa na mtoto pamoja ambaye Harmonize alijaribu kuficha kwa kipindi cha miezi saba ili kuokoa ndoa yake na Sarah.

Ingawa sio mengi yanayojulikana kuhusu mahusiano ya Harmonize na Shanteel, ni wazi kuwa ndiyo yalisababisha kuvunjika kwa ndoa ya mwanamuziki huyo na Sarah.

Kajala Masaja

Harmonize na Frida Kajala
Harmonize na Frida Kajala
Image: HISANI

Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masaja walichumbiana kwa kipindi kifupi kati ya mwaka wa 2020 na 2021.

Wawili hao waliweka mahusiano yao wazi mwezi Februari mwaka huu ingawa tayari walikuwa wameanza kuchumbiana mapema kabla ya kujitokeza.

Miezi miwili tu baada ya wasanii hao wawili wabongo kujitokeza kama wapenzi mahusiano yao yalifika kikomo katika hali tatanishi.

Walipokuwa kwenye mahusiano, Harmonize na Kajala walikuwa wamechora tatoo za majina yao ili kuashiria mapenzi makubwa kati yao. Hata hivyo wote wawili walifuta tatoo hizo baada ya kutengana.