Harmonize aeleza kwa nini angali na tattoo ya Diamond kwenye mkono wake licha ya ugomvi wao

Muhtasari

•Harmonize alisema licha ya uhasama mkubwa kati yao uliojionyesha wazi miaka ya hivi karibuni bado angali na heshima kubwa kwa aliyekuwa bosi wake katika lebo ya Wasafi.

•Konde Boy alisema alipokuwa anachora tattoo ile alitaka iwe kumbukumbu kuwa Diamond alimuinua kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Harmonize
Harmonize
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize angali amehifadhi tattoo ya bosi wake wa zamani Diamond Platinumz licha yake kugura label ya WCB  zaidi ya miaka miwili iliyopita baada ya kutofautiana kwa muda.

Hivi majuzi mzaliwa huyo wa eneo la Mtwara alipokuwa anahutubia waandishi wa habari punde baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani alionyesha tatoo hiyo ya sura ya Diamond iliyo kwenye kifundo cha mkono wake kushoto.

Harmonize alisema licha ya uhasama mkubwa kati yao uliojionyesha wazi miaka ya hivi karibuni bado angali na heshima kubwa kwa aliyekuwa bosi wake katika lebo ya Wasafi.

"Licha ya yote, mimi nina heshima kubwa kwake. Leo hii licha ya makelele yote unayosikia niko na tatoo ya Diamond. Hii ni sura yake. Licha ya yote!" Harmonize alisema.

Konde Boy alisema alipokuwa anachora tattoo ile alitaka iwe kumbukumbu kuwa Diamond alimuinua kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Alisema licha ya yote hana nia ya kuifuata ila uhusiano wao ukiendelea kudhoofika zaidi  huenda akafanya maamuzi ya kuifuta.

"Wakati nilichora hii tattoo nilijua kuwa aliniinua kutoka sehemu moja hadi nyingine.Sisi ni vijana. Nilijua huenda siku ikafika tusifanye kazi pamoja. Hii itakuwa kama kumbukumbu kwenye moyo wangu. Ndio maana hata leo sijaifuta na sina mpango wa kuifuta. Lakini kwa jinsi tunavyoendelea mbele. Nitaona mtu ambaye ako tayari wewe ufe nitakuwa naye wa nini sasa?!!" armonize alisema.

Miaka miwili iliyopita uvumi kwamba Harmonize alikuwa amefuta tattoo ya Diamond baadaya kugura Wasafi ulienea kote mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Mmiliki huyo wa Konde Music Worldwide alisema kabla yake kutoka Wasafi alikuwa amejaribu sana kurejesha uhusiano mzuri na Diamond.

Alisema amesikitika sana kuona watu wanaendelea kumhukumu vibaya na kumuona kama msaliti ilhali hawana ufahamu wa kilichomsukuma kutoka kwa lebo iliyoinua taaluma yake ya muziki ya Wasafi.