Diamond Platnumz adai alitumia zaidi ya Sh.8.7 milioni kwenye harusi ya marafiki zake

Muhtasari
  • Diamond Platnumz adai alitumia zaidi ya Sh.8.7 milioni kwenye harusi ya marafiki zake
Diamond Platnumz
Image: Hisani

Diamond Platnumz alimzawadia rafiki yake, Aristotee na mkewe Emmy; pesa, mali na matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya harusi yao, yote yakiwa ni Sh.8.7 milioni.

Aristotee Kagombe ni mtu maarufu nchini Tanzania ambaye anasifika kwa kutoa maoni yake kila mara kuhusu masuala yanayovuma nchini.

Pia anajulikana kwa kukosoa chochote na mtu yeyote bila woga.

Jumamosi, Novemba 20, wanandoa hao walifanya sherehe kubwa ambayo ilianza na harusi ya kanisani kisha ikamalizika kwa hafla ya mapokezi usiku kucha.

Harusi hiyo ambayo ilikuwa kubwa ilionyeshwa moja kwa moja na  runinga ya Wasafi, kituo cha habari kinachomilikiwa na Diamond Platnumz.

Mapema Jumapili, Novemba 21, staa huyo wa Bongo Flava alitumia ukurasa wake wa Instagram kuweka wazi kiasi alichotumia kufanikisha siku kuu ya rafiki yake huyo.

Platnumz alifichua kuwa aliwazawadia wanandoa hao Sh728,000 (TZS15 milioni), hundi nyingine ya wazi ya Sh728,000, kipande cha ardhi chenye thamani ya Sh2.4 milioni (TZS50 milioni). Pamoja na matangazo ya moja kwa moja ya saa 5 kwenye Wasafi TV ambayo yanagharimu Sh4.8 milioni (TZS100 milioni).

Katika hotuba yake kuhusu harusi hiyo, Platnumz alisema alifanya hivyo kutokana na mapenzi aliyonayo kwa rafiki yake huyo ambaye amekuwa msaidizi wake mkubwa.