"Mahusiano yetu hayakuwa yamepangwa" Guardian Angel na Esther Musila wazungumzia safari yao ya mapenzi

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watatu alisema hakuwahi kadiria ingefikia wakati waanze kuchumbiana kwani huo haukuwa mpango wao.

•Guardian Angel alisema maisha yake yamebadilika sana tangu walipojitosa kwa ndoa huku akieleza mkewe amemsaidia sana kimawazo na katika taaluma yake ya muziki.

•Hata hivyo Musila alikiri waliogopa kufichulia watoto wake kuhusu mahusiano yao kwani walikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi wangeichukulia.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mwanamuziki Guardian Angel na mpenzi wake Esther Musila wamefunguka kuhusu jinsi hali imekuwa katika kipindi cha takriban miaka miwili ambayo wamekuwa kwenye mahusiano.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, bi Musila alisema alipokuwa anajuana na Guardian Angel alikusudia kumsaidia katika muziki wake kwani alihisi hakuwa amefikia kilele ambacho anastahili na alikuwa na mengi ambayo hayakuwa yamefumbuliwa.

Mama huyo wa watoto watatu alisema hakuwahi kadiria ingefikia wakati waanze kuchumbiana kwani huo haukuwa mpango wao.. Alisifia sana mapenzi makubwa ambayo mwanamuziki huyo amekuwa akimpatia tangu walipojitosa kwenye mahusiano

"Ni yeye tu! Mahusiano haya hayakuwa yamepangwa. Nadhani mioyo yetu iliunganishwa tu kabisa. Wakati mwingine huwa namwangalia najiuliza tumefikaje tulipo. Yeye ni mtu spesheli. Ana moyo mzuri zaidi. Sijawahi pendwa hivi. Huwa inajileta tu. Sio mambo ambayo unafanya ili kuonyeshana tu. Ananionyesha mapenzi hata tukiwa kwa nyumba. Naishi maisha yangu bora zaidi" Bi Musila alisema.

Guardian Angel kwa upande wake alisema ilikuwa rahisi kwake kumruhusu Bi. Musila maishani mwake, jambo ambalo si kawaida yake.

Alisema maisha yake yamebadilika sana tangu walipojitosa kwa ndoa huku akieleza mkewe amemsaidia sana kimawazo na katika taaluma yake ya muziki.

"Amenifanya mtu bora. Nimepata utulivu wa akili. Sasa naweza kufikiria vizuri. Nimeweza kufanikiwa katika mambo ambayo kwa  miaka mingi sikudhani ningewezakufanya. Akili yangu imebadilika na ni tulivu. Ananisaidia kuwa mwenye adabu,kuheshimu kazi yangu na kutia bidii kwani ananishinikiza kufikia mahali anataka" Guardian Angel alisema.

Musila alisema tayari ametambulisha mpenzi wake kwa wanafamilia wake wa karibu ikiwemo  watoto wake watatu, ndugu yake pamoja na familia yake.

Hata hivyo Musila alikiri waliogopa kufichulia watoto wake kuhusu mahusiano yao kwani walikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi wangeichukulia.

'Tuliogopa kwa sababu hatukujua jinsi watoto wangu wangeichukulia. kwa sababu nimekuwa mzazi wao wa pekee kwa muda. Ilikuwa ngumu mwanzoni lakini walikuja kukubali polepole. Sasa tuko sawa" Alisema Musila.

Musila hata hivyo alisema bado hajaweza kupatana na familia ya Guardian Angel kwani mama yake anaishi Canada