"Kuwa single mama sio cheo au ulemavu!" Akothee ajivunia kusomesha bintiye Rue Baby hadi kuhitimu katika chuo kikuu pekee yake

Muhtasari

•Ameweka wazi kuwa amebeba jukumu la kumsomesha bintiye na kumpa mahitaji ya kimsingi pekee yake bila usaidizi huku akisema ana furaha tele kuona jasho lake limezaa matunda.

•Amempongeza Rue Baby kwa kuwajibika na fedha za shule huku akifichua amekuwa akimkabidhi bintiye jukumu la kufanya malipo yote katika kipindi ambacho amekuwa akisoma.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu kama Akothee amesherehekea kuhitimu kwa mtoto wake wa Pili anayefahamika kama Rue Baby.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 amesema amewezwa na hisia kuona ameweza kumsomesha mtoto wake mwingine hadi kuhitimu katika chuo kikuu.

Ameweka wazi kuwa amebeba jukumu la kumsomesha bintiye na kumpa mahitaji ya kimsingi pekee yake bila usaidizi huku akisema ana furaha tele kuona jasho lake limezaa matunda.

"Kuwa mama singo sio cheo ama ulemavu. Ni simulizi ya safari ya mafanikio ya mama aliyejiinua kuchukua majukumu yote ya wazazi wote wawili ikiwemo aliyekosa. Kutoa mahitaji yote ya kimsingi kwa watoto wake na kuunda mazingira mazuri kwa ukuaji wa afya wa mtoto. Ninaoneka mwenye sarakasi mitandaoni lakini nimeweka mambo yangu vizuri.  Ni safari ya single mother kwangu. Leo nitaongea kwa ufupi sana maana nina hisia sana. Siwezi kuamini niko kwenye digrii yangu ya Pili na @rue.baby, peke yangu!!" Akothee ameandika.

Mama huyo wa watoto watano amempongeza Rue Baby kwa kuwajibika na fedha za shule huku akifichua amekuwa akimkabidhi bintiye jukumu la kufanya malipo yote katika kipindi ambacho amekuwa akisoma.

Amesema anawapenda watoto wake sana huku akimshukuru bintiye kwa kutomletea aibu nyumbani na kufanya ulezi uwe rahisi kwake. 

"Hakuna mtu aliyewahi kuuliza kama ninahitaji msaada, yote yalionekana kupendeza.  Hongera sana mpenzi wangu. Umenirahisishia uzazi, umeelewa kazi yako na umeleta zawadi. Mimi ni mama yako @rue.baby. Mungu akiniomba kundi jingine la watoto, bado nitachagua wewe na ndugu zako.

Sijui shule hii iitwayo Strathmore iko wapi! Sijui hata maelezo ya akaunti wala benki wanayotumia. Ninahamisha pesa kwenye akaunti yako kwa nikitumai aidha utachagua kutumia au kulipia maisha yako ya usoni! HONGERA! HONGERA SANA! HONGERA SANA! HONGERA SANA @rue.baby" Akothee amesema.

Haya yanajiri takriban mwaka mmoja tangu tu tangu kifungua mimba wa Akothee, Vesha Okello kuhitimu kutoka chuo kikuu.