Papa Francis alaani unyanyasaji wa nyumbani kama 'karibu na ushetani'

Muhtasari
  • Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki alisema hayo wakati wa kipindi kilichotangazwa kwenye mtandao wa TG5 nchini Italia siku ya Jumapili
pop
pop

Papa Francis amelaani unyanyasaji wa majumbani dhidi ya wanawake kama "unaokaribia ushetani' katika mojaapo ya lugha yake kali zaidi kuhusu suala hilo.

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki alisema hayo wakati wa kipindi kilichotangazwa kwenye mtandao wa TG5 nchini Italia siku ya Jumapili.

Alizungumza na jopo la watu wanne kutoka asili mbali mbali ikiwa ni pamoja na manusura wa unyanyasaji wa nyumbani.

Alilalamikia "idadi kubwa sana" ya wanawake "wanaopigwa na kunyanyaswa majumbani mwao."

"Tatizo ni kwamba, kwangu, ni karibu na jambo la kishetani kwa sababu ni kutumia fursa ya kumuangamiza mtu ambaye hawezi kujitetea, ambaye anaweza tu [kujaribu] kuzuia mapigo," Papa Francis alisema. "Inafedhehesha. Inafedhehesha sana."

Alizungumza na mwanamke anayeitwa Giovanna ambaye alisema alikuwa ametoroka katika ndoa yenye mateso pamoja na watoto wake wanne.

Papa aliongeza kuwa wanawake waliodhulumiwa hawajapoteza utu wao.

"Naona heshima kwako kwa sababu kama huna hadhi, usingekuwepo hapa," alimwambia Giovanna. "Angalia Mama Mbarikiwa na ukae na picha hiyo ya ujasiri."

Tangu kuanza kwa janga la Covid, Papa Francis ametoa maoni kadhaa juu ya unyanyasaji wa nyumbani.

Matukio ya unyanyasaji yameongezeka katika nchi kadhaa, kwani watu wengi wamenaswa na wanaowanyanyasa wakati wa marufuku za kutotoka nje

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyohusisha nchi 13, nusu ya wanawake waliohojiwa walisema wamekumbwa na aina fulani ya ukatili tangu kuanza kwa janga hilo.

Nchini Italia, takwimu za polisi zilizotolewa mwezi uliopita ziliripoti karibu matukio 90 ya unyanyasaji dhidi ya wanawake kila siku - 62% ya haya yalikuwa kesi za unyanyasaji wa nyumbani.

Akihutubia Giovanna, Papa Francis alisema inawezekana bado kuwa na matumaini, hata wakati wa janga hilo.

"Unatoa mfano wa kupambana na hali ngumu, somo la kupinga majanga," alisema. "Unajitokeza vizuri zaidi kuliko hapo awali."