"Pafu moja limeanguka tayari!" Taarifa zaidi kuhusu ugonjwa wa Akuku Danger zatolewa, familia yaomba msaada

Muhtasari

•Silprosa ambaye ni mwandani wa Akuku Danger mkubwa alisema afya yake si nzuri hata kidogo na kueleza kuwa pafu lake moja limeathirika vibaya.

•Familia na marafiki wa Akuku wametoa ombi la msaada wa kifedha kwa Wakenya ili kuweza kugharamia matibabu ghali ya msanii huyo.

Image: INSTAGRAM/ SANDRA DACHA

Mchekeshaji wa Churchill Show Mannerson Oduor Ochieng almaarufu kama Akuku Danger anaugua vibaya na anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Nairobi Women’s Hospital.

Baadhi ya wasanii mashuhuri ikiwemo Daniel ‘Churchill’ Ndambuki, Terence Creative, Sandra Ndacha (Silprosa) na Milly Chebby walienda kumtembelea msanii huyo mwenzao hospitalini siku ya Alhamisi na wakatoa taarifa zaidi kuhusu afya yake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Silprosa ambaye ni mwandani wa Akuku Danger mkubwa alisema afya yake si nzuri hata kidogo na kueleza kuwa pafu lake moja limeathirika vibaya. Alifichua kwamba hii ni mara ya pili msanii huyo kulazwa hospitalini katika kipindi cha wiki moja.

“Nimekubali uhai ni Mungu tu anapeana, haendelei vizuri sana. Pafu lake moja limeanguka na kwa sasa anapigania maisha yake ICU!” Sandra alisema.

Mwigizaji huyo wa Auntie Boss ameomba Wakenya kumkumbuka Akuku Danger katika maombi yao.

Familia na marafiki wa Akuku wametoa ombi la msaada wa kifedha kwa Wakenya ili kuweza kugharamia matibabu ghali ya msanii huyo.

“Akuku Danger alilazwa katika hospitali ya Nairobi Women's - Rongai wiki jana na kuruhusiwa kuenda nyumbani. Alipewa dawa na sasa amelazwa tena. Pafu lake moja limeanguka na sasa ako ICU. Anafaa kuhamishwa kupelekwa Nairobi West Hospital hivi karibuni na wanataka 200,000. Tunawaomba marafiki watusaidie kuongeza kiasi. Kwa sasa laini ya mchango ni 0713792757(Nelson Hosea)” Ujumbe uliochapishwa na Terence Creative kwenye ukurasa wake wa Instagram ulisoma.