'Sikuwa tayari kwa kuondoka kwako,' Wahu amkumbuka marehemu babake kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo amesema anatamani sana baba yake angekuwa hai bado  ili aone jinsi angehusiana na wajukuu wake.

•Amemsifia sana babake kwa kuwa mzazi bora huku akimtaja kama mto mwenye upendo, mkarimu, mwenye heshima na mwaminifu.

Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Mwanamuziki mashuhuri nchini Wahu Kagwi ameadhimisha miaka tisa tangu baba yake, GS Kagwi  alipoaga dunia.

Mnamo Jumanne, mke huyo wa Nameless alitumia ukurasa wake wa Facebook kumwandikia baba yake ujumbe maalum wa kihisia kuashiria jinsi alivyomthamini.

Katika chapisho lake, mwanamuziki huyo alisema anatamani sana baba yake angekuwa hai bado ili aone jinsi angehusiana na wajukuu wake.

"Mara nyingi huwa najiuliza kama baba angekuwa hapa, je uhusiano wake na watoto wangu ungekuwaje? Karibu naona Tumiso wangu akiongea na wewe kuhusu wavulana anaowapenda na kukushirikisha ndoto zake kubwa na matamanio yake (wavulana na ndoto zilikuwa mada ulizozikubali!!! sasa kwa kuwa mimi ni mzazi, naelewa kwanini. Nzuri baba! ) Naona ukimsisimua Nyakio kipuuzi na akikoroma kwa nguvu huku akikimbia. Nashangaa jinsi uhusiano wako na Monski ungekua, na iwapo hatimaye angejifunza jinsi ya kuelezea miundo ya majengo kwa Kikuyu" Wahu aliandika.

Wahu alikumbuka nyakati nzuri alizokuwa nazo pamoja na marehemu babake huku akieleza jinsi alivyozifurahia na kuzithamini.

Alimsifia sana babake kwa kuwa mzazi bora huku akimtaja kama mto mwenye upendo, mkarimu, mwenye heshima na mwaminifu.

"Hukuwa tajiri wa fedha, dhahabu au mali ya dunia, lakini kwa upendo, wema, uaminifu na heshima, utajiri wako ulikuwa usio na kipimo. Sikuwa tayari wewe kuondoka, lakini ilibidi. Ni ukweli mchungu wa maisha. Hata kama ulioondoka kimwili, unaishi kwenye mioyo yetu na  kumbukumbu zetu. Asante kwa kuwa baba mzuri kwetu. Endelea kupumzika kwa amani. Miaka 9 imepita, tunakumbuka, na tutakupenda daima. endelea kupumzika kwa amani" Aliandika Wahu.

Mama huyo wa wasichana wawili alimpoteza baba yake mwaka wa 2013.