Gwiji wa Taarab kutoka Zanzibar Khadija Omar Kopa amesema hana ufahamu wowote iwapo binti yake Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu anapanga ndoa na bosi wake Diamond Platnumz.
Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Bi Kopa alieleza kwamba hafahamu iwapo kuna mahusiano ya kimapenzi kati ya binti yake na bosi huyo wa WCB.
Hata hivyo, Kopa alisisitiza kwamba bintiye ametosha mboga kuchukua nafasi ambayo hapo awali ilikuwa imekaliwa na walimbwende tajika kama Zari Hassan, Wema Sepetu, Hamissa Mobetto, Tanasha Donna, kati ya wengine.
"Mimi sijui kama Zuhura yuko na Diamond. Lakini, mwanamke ni mwanamke. Zuhura ni mwanamke aliyefundishika. Mwanamume mwenye kutaka mke, hutafuta mwanake wanayelingana kitabia. Usije ukamwona Zuhura mdogo wa mwili, lakini mkubwa wa mambo. Pengine ulimi wake mzuri, anazungumza vizuri. Pengine anaishi na mtu kwa wema, anajua mahaba, hayo ndio mambo wanaume wanataka. Usidharau binti yangu ukamwona mdogo, yule mtoto wa Kizanzibari amelelewa kwenye maandhari ya mahaba na mapenzi" Kopa alisema.
Mtunzi huyo mahiri wa Taarab alisema hatakuwa na tatizo lolote iwapo Zuchu ataamua kujitosa kwa ndoa na Diamond na kueleza kwamba ako tayari kumuozesha bintiye.
Kopa alisema ako tayari kumkubali mwanaume yeyote ambaye Zuchu atachagua kama mchumba huku akisisitiza kwamba furaha ya bintiye ndiyo kipaumbele.
"Mwanamume yeyote tu ambaye watapendana, mimi niko na furaha ya mwanangu. Nataka awe na furaha. Sisi tunajali furaha ya mwanawe. Mwanaume awe nacho au asiwe nacho, najali furaha ya mwanangu.Sisi kwetu maskini lakini roho zetu tajiri" Kopa alisema.
Bi Kopa alipoulizwa iwapo ni kweli baba wa kambo wa Diamond, Uncle Shamte, meneja Ricardo Momo na wazee kutoka upande wa Diamond waliamtembelea Zanzibar kupeleka barua ya uchumba alisema kwamba ni kweli walifika ila akasusia kufichua sababu zao kumtembea.
Kopa alisisitiza kwamba Februari 14 itakuwa siku kubwa kwa binti yake na mengi yatafichuka kumhusu.