"Anapigania maisha yake kitandani!" Familia ya Professor Jay yaomba msaada wa matibabu

Muhtasari

•Rapa huyo ambaye amekuwa akitumbuiza kwa miaka mingi alilazwa takriban wiki tatu zilizopita akiwa hali mahututi.

•Familia ya Jay ambaye pia ni mwanasiasa hata hivyo imesalia kimya kuhusu ugonjwa ambao unamuathiri.

Mwanamuziki Joseph Haule almaarufu kama Profesa Jay
Mwanamuziki Joseph Haule almaarufu kama Profesa Jay
Image: HISANI

Nyota wa muziki kutoka Tanzania Joseph Leonard Haule almaarufu kama Professor Jay anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Muhumbili baada ya kushikwa na a na maradhi wiki kadhaa zilizopita.

Taarifa kutoka Bongo zinasema kuwa rapa huyo ambaye amekuwa akitumbuiza kwa miaka mingi na pia kuhudumu kama mbunge alilazwa takriban wiki tatu zilizopita akiwa hali mahututi.

Familia na marafiki wa Jay sasa wametoa wito wa msaada wa kifedha kutoka kwa wasamaria wema ili kugharamia matibabu yake.

Kupitia chapisho la Facebook, mwanamuziki Mwana FA amesihi wasamaria wema kusaidia kuchanga fedha za matibabu ya Jay ambayo yanasemekana kuwa ghali sana. Mwana FA amefichua kwamba afya ya rapa huyo imeendelea kudhoofika.

Kaka yangu @professorjaytz anapigania maisha yake kitandani..kaka yangu ni mgonjwa. Hakuna asiyejua makubwa aliyoyafanya kwa mziki wetu. Alitunyooshea sana njia,yeye peke yake..akatubadilishia uelekeo kabisa na mziki wetu ukakosa mipaka,si kwa rika si kwa jinsia,ukawa wa kila mmoja.Binafsi sina cha kumlipa kwa ‘uongozi’ wake wa moja kwa moja ama wa mbali kwangu.

Nawaomba tu tuonyeshe mapenzi yetu kwa kuchangia matibabu yake ambayo gharama yake ni kubwa MNO..Tujitoe kuokoa maisha ya MC bora wa muda wote nchi hii, @professorjaytz Mwalimu wa wengi." Mwana FA alisema.

Familia ya Jay ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Mikumi hata hivyo imesalia kimya kuhusu ugonjwa ambao unamuathiri.

Mchango unatolewa kupitia MPESA 0757919192, TiGOPesa 0715 919 192, na CRDB acc no: 0112044845200 Joseph Leonard Haule.