Mama Baha afunguka kuhusu masaibu ya familia yake baada ya kakake kutekwa nyara Somalia

Muhtasari

•Wanjiku alisema hawajafanikiwa kuona kaka yake George tangu mwaka wa 2013 ambapo alitekwa nyara mjini Mogadishu, Somalia.

•Familia haijawahi pata kufahamu nini hasa kilichomtokea kakake kwani hakujakuwa na mawasiliano yoyote katika kipindi hicho cha miaka tisa ambacho hajakuwepo.

•Alifichua kuwa amechorwa tattoo za jina la kakake mkononi na shingoni kama ishara ya upendo mkubwa ambao anao kwake.

Image: INSTAGRAM// WANJIKU MBURU

Mwigizaji mashuhuri Wanjiku Mburu almaarufu kama Mama Baha kutokana na kipindi cha Machachari amefunguka kuhusu masaibu yaliyokumba familia yake baada ya ndugu yake kutekwa nyara takriban miaka tisa iliyopita.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Wanjiku alisema hawajafanikiwa kuona kaka yake George tangu mwaka wa 2013 ambapo alitekwa nyara mjini Mogadishu, Somalia.

Mwigizaji huyo alisema tukio hilo limemuathiri kwa miaka mingi kwani kulikuwa na uhusiano wa karibu kati yake na kakake aliyetekwa nyara ambaye ndiye pekee aliyekuwa amesalia hai kati ya ndugu zake watatu.

"Katika maisha yangu yote nikitaka kufanya chochote yeye ndiye nilikuwa napigia simu. Tangu tukiwa wadogo tulikuwa karibu sana naye. Ndugu zangu wengine walifariki kitambo. Kakangu mkubwa alifariki nikiwa katika darasa la sita na mwingine baada ya kumaliza kidato cha nne. Joji pekee ndiye nilibaki naye, tungefanya mambo mengi pamoja" Wanjiku alisema.

Wanjiku alisema familia haijawahi pata kufahamu nini hasa kilichomtokea kakake kwani hakujakuwa na mawasiliano yoyote katika kipindi hicho cha miaka tisa ambacho hajakuwepo.

Alisema familia yake imekuwa ikiishi kwa matumaini kwamba siku moja kakake aliyepotea atarudi na kufufua furaha ambayo hawajakuwa nayo kwa miaka mingi.

"Ata kama alikuwa amefanya makosa mahali akafungwa jela, sidhani angekuwa amekaa miaka hiyo yote. Saa hii angekuwa amemaliza. Kwa familia  na watoto wake, nadhani miaka tisa ni mingi sana..

Natumai kuwa matumaini niliyo nayo yanawezwa kusambazwa kwake pia na aendele kujua kuwa tukonaye kila wakati. Tunapambana, tunajaribu kila kitu tutakachoweza ili kumrejesha" Alisema.

Mwigizaji huyo alisema angetamani kufahamu hatima ya kakake  kwa kuwa kila siku huwa anamkumbuka na kumpeza sana.

Wanjiku pia alifichua kuwa amechorwa tattoo za jina la kakake mkononi na shingoni kama ishara ya upendo mkubwa ambao anao kwake.