Nitalipa madeni ya china kutumia gunia 50 za bangi- Mgombeaji urais Profesa Wajackoyah

Muhtasari

•Wajackoyah alieleza kuwa lengo lake kuu sio kuhalalisha matumizi ya bangi hapa nchini ila kuhalalisha ukulima wa bangi ya kuuza nje ya nchi.

•Wajackoyah pia alitangaza kuwa endapo atachaguliwa kama rais Wakenya watafanya kazi siku nne pekee kwa wiki.

Profesa George Wajackoyah
Profesa George Wajackoyah
Image: HISANI

Kiongozi wa Roots Party Prof George Wajackoyah amesisitiza kwamba atahalalisha mmea wa bangi iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Kenya katika chaguzi kuu za mwezi Agosti.

Akiwa kwenye mahojiano na mchekeshaji Victor Naman, Wajackoyah alieleza kuwa lengo lake kuu sio kuhalalisha matumizi ya bangi hapa nchini ila kuhalalisha ukulima wa bangi ya kuuza nje ya nchi.

Mzaliwa huyo wa kaunti ya Kakamega alisema anapanga kutumia mapato yatakayotokana na mauzo ya bangi kulipa madeni makubwa ya Kenya kwa mataifa mengine.

"Bangi itahalalishwa kwa mauzo ya nje ndio tulipe madeni ya China. Matumizi ya kujiburudisha yatakuwepo ingawa yatadhibitiwa. Gunia moja ya bangi huenda ikagharimu dola milioni 3.4. Nitalipa China madeni ya babaraba kwa takriban gunia hamsini za bangi" Wajackoyah alisema.

Kulingana na profesa huyo, mmea wa bangi una matumizi mengi  ikiwemo kutibu saratani, kutengeneza chakula, mafuta, kamba na mbolea. 

Wajackoyah pia alitangaza kuwa endapo atachaguliwa kama rais Wakenya watafanya kazi siku nne pekee kwa wiki.

"Watu watafanya kazi siku nne pekee ili Waislamu wawe na siku yao ya maombi sio kupewa saa moja tu ya kufanya maombi. Hizo siku nne tutazipangia vizuri ili watu waweze kuwa na tija zaidi" Alisema.

Mgombeaji huyo wa urais alitangaza kuwa chama chake cha Roots Party hakitabagua mwanasiasa yeyote atakayetaka kujiunga nacho.

Alidai kwamba kabla hajakuwa wakili aliwahi kuwa chokora, mlinzi wa lango, mchimba kaburi na afisa wa polisi.