Tamasha ya kutoa tuzo za mwaka huu za I Heart Radio Music Awards ilifanyika usiku wa Jumanne katika ukumbi wa Shrine Auditorium jijini Los Angeles nchini Marekani ambapo wasanii mbalimbali walijinyakulia tuzo katika vitengo tofauti tofauti.
Tukio kubwa zaidi ni lile la msanii nguli wa hiphop, Drake kushinda tuzo ya msanii bora wa mwaka wa 2022 katika kitengo cha hiphop kwa kuwabwaga Lil Baby, Megan Thee Stallion, Moneybagg Yo na Pop Smoke.
Katika kitengo cha msanii wa kiume bora wa mwaka, Lil Nas X alibeba siku mabegani kwa kuibuka mshindi mbele ya mastaa wengine kama Ed Sheeran, Drake na Justin Bieber waliokuwa wakimenyana katika kitengo hicho.
Bara la Afrika pia lilipata uwakilishwaji japo finyu ambapo collabo ya Wizkid na Tems ilishinda katika kitengo cha ngoma bora ya Hiphop ya mwaka.