Diamond Platnumz amvulia kofia mchora katuni wa Tanzania aliyetengeneza gari la umeme

Muhtasari

•Diamond Platnumz amesema gari hilo sio fahari kwa Kipanya tu bali pia kwa Jamhuri yote ya Tanzania.

•Kipanya alitengeneza gari hilo mwenyewe kupitia kampuni yake ya Kaypee Motors. Ilimchukua muda wa miezi 11 kulikamilisha gari hilo alilopea jina KP A72 ev.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ, MASOUD KIPANYA

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu kama Diamond Platnumz amependezwa sana na ubunifu wa mchora katuni mmoja wa  Tanzania ambaye alitengeneza gari ndogo linalotumia nguvu za umeme.

Siku ya Jumamosi, mchora katuni Masoud Kipanya alizindua gari la kwanza la umeme kutengenezewa nchini Tanzania.

Diamond ambaye anaaminika kuwa msanii mkubwa zaidi Bongo amesema gari hilo sio fahari kwa Kipanya tu bali pia kwa Jamhuri yote ya Tanzania.

"Najivunia wewe ndugu yangu Masoud Kipanya. Gari hiii ni fahari si kwako tu, bali ni kwa taifa zima la Tanzania," Diamond alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Bosi huyo wa Wasafi alisema ubunifu wa Masoud ni wa kutia motisha kwa vijana wa Bongo na unaweka nchi hiyo jirani katika nafasi nzuri ya kutambulika kote duniani.

"Rai yangu kwa Watanzania, tuunge mkono kwa wingi juhudi hii, maana ni wakati wa kujivunia bidhaa zetu sasa," Diamond alisema.

Kipanya alitengeneza gari hilo mwenyewe kupitia kampuni yake ya Kaypee Motors. Ilimchukua muda wa miezi 11 kulikamilisha gari hilo alilopea jina KP A72 ev.