Rev Victor Githu azungumzia madai ya kuchumbia mwanadada mjamzito wa miaka 25

Muhtasari

•Victor aliweka wazi kuwa angali na umri mdogo na hajakomaa kufika hatua mwafaka ya kuwa kwa mahusiano.

Image: FACEBOOOK//VICTOR GITHU

Mchungaji mdogo zaidi kwa umri nchini Kenya Victor Githu amepuuzilia mbali tetesi kuwa amewahi kuwa kwenye mahusiano na mwanadada aliyemzidi umri zaidi ya mara dufu. 

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Victor alisema ripoti zilizosema kuwa anachumbiana na mwanadada mjamzito mwenye umri mwenye umri wa miaka 25 ni za uwongo.

Mwanafunzi huyo wa darasa la saba aliweka wazi kuwa angali na umri mdogo na hajakomaa kufika hatua mwafaka ya kuwa kwa mahusiano.

"Mbona sasa? Mimi bado ni mdogo sana, bado nakua. Watu wanatunga hadithi wakijaribu kuniharibia jina kwa kuwa nimeokoka. Wakati wengine Wakenya huwa wananihukumu na kupigana nami kwa kuwa wamesikia maneno. Lakini wanafaa wajiulize, mtoto wa miaka 10-11-12 atawezaje kuwa na mke au mchumba mwenye miaka 25? Watu wanakosa maarifa. Hakuna mwenye atawahi fanikiwa kuniharibia jina," Victor alisema.

Mtumishi huyo pia alipuuzilia mbali madai kuwa  yeye ni mhubiri mdanyanyifu anayenuwia kuwalaghai waumini wake.

"Jina la injili liliharibiwa. Tuache kuhukumu lakini, sio kila mtu ni mbaya.  Kuna walaghai ndio. Wao wako kwa tasnia, mimi niko kwa huduma. Kwa tasnia unategemea watu wakulipe, lakini kwa huduma unategemea Mungu. Mimi sio mdanyifu chipukizi," Alisema.

Victor alifichua kuwa anapanga kuanzisha kanisa la kimataifa baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu. Pia alisema anatazamia shirika la hisani ili kusaidia watu wasiojiweza.