Niliona mwanga ukimulika usiku nikaanza kupona- King Kaka asimulia safari ya kupona kwake

Muhtasari

•King Kaka alifichua kuwa hamu yake ya chakula imerejea kikamilifu na tayari ameongeza uzito mwilini.

•Kaka alisema aliona mwangaza mkali na punde baada ya hilo akaanza kupata afueni na hamu yake ya kula ikarejea.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwimbaji wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu King Kaka ametangaza wazi kuwa afya yake tayari imeimarika.

Akiwa kwenye mazungumzo na Jalang'o, King Kaka alifichua kuwa hamu yake ya chakula imerejea kikamilifu na tayari ameongeza uzito mwilini.

"Saa hii niko poa. Nakula kama fala saa hii, kila saa. Nilishaongeza kilo," King Kaka alisema.

Mwanamuziki huyo alisema mwili wake uliathirika vibaya baada ya kupimwa vibaya na kupewa dawa zisizofaa.

Alisema uzito wake wa mwili ulishuka kutoka kilo 86 hadi 53 kwa kuwa hata hakula anakula chochote alipokuwa anaugua.

"Nilikuwa nimekata kilo. Hata kuona sasa naweza kukaa chini ni baraka. Sikuwa naweza kukaa. Sikuwa naweza kutembea, nilikuwa nahisi uchungu nikikaa. Ilifika wakati ikabidi nimeenda hospitali," Alisema.

King Kaka alifichua kuwa alianza kupata afueni baada ya Mungu 'kumtembelea' usiku mmoja akiwa amelazwa hospitalini.

Alisema aliona mwangaza mkali na punde baada ya hilo akaanza kupata afueni na hamu yake ya kula ikarejea.

"Nilikuwa kwa giza. Mwangaza ukatokea usiku. Baada ya hilo nilianza kupona tu. Sikuwa nimekula wiki moja. Siku iliyofuata nilikunywa uji," Alisema King Kaka.

Msanii huyo amesema kwa sasa amepona kikamilifu na tayari amerudi kwenye kazi zake za usanii.

Alifichua kuwa kwa sasa anatengeneza albamu mpya pamoja na ngoma zingine kadhaa ambazo atakuwa anaachia hivi karibuni.

Mwaka jana King Kaka aliugua kwa zaidi ya miezi minne. Ugonjwa uliokuwa umemshambulia ulimwathiri hadi kufikia kulazwa hospitalini.

Katika kipindi hicho alipoteza zaidi ya kilo 33, rangi ya midomo yake ikabadilika miongoni mwa dalili zingine za kutisha.