"Anajipiga kifua sana!" Ringtone Apoko ataja sababu zake kusukuma kesi ya dhuluma dhidi ya Alai

Muhtasari

•Ringtone alisisitiza kuwa ataendelea kuhudhuria vikao vya mahakama hadi  wakati ambapo uamuzi utatolewa.

•Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa lengo lake sio kulipiza kisasi bali ni kuona haki imetendeka.

Ringtone Apoko, Robert Alai
Ringtone Apoko, Robert Alai
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji wa nyimbo za injili Ringtone Apoko ameapa kuendelea kusukuma kesi ya dhuluma dhidi ya mwanablogu Robert Alai licha ya changamoto chungu alizokumbana nazo mahakamani.

Akizungumza Jumatatu baada ya kesi hiyo kuahirishwa kwa mara nyingine, Ringtone aliweka wazi kuwa lengo lake sio kulipiza kisasi bali ni kuona haki imetendeka.

"Nafanya hii kesi ili yule mtu mrefu aheshimu mtu mfupi, yule mtu mnene aheshimu mtu mwembamba, yule mtu ako na pesa aheshimu mwenye hana," Ringtone alisema akiwa kwenye mahojiano na Nicholas Kioko.

Mwanamuziki huyo aliyezingirwa na drama si haba alilalamika kuhusu jinsi kesi hiyo ambayo aliwasilisha Julai mwaka jana inaendeshwa.

Hata hivyo alisisitiza kuwa ataendelea kuhudhuria vikao vya mahakama hadi  wakati ambapo uamuzi utatolewa.

"Hata akisongesha mara ngapi, tuko. Mimi labda waniue lakini niko. Nitakuwa nakuja wa kwanza kortini. Labda wanaona nipo bizi wanadhani eti sitakuja, nitakuja kortini," Alisema.

Msanii huyo alimshtumu Alai kwa kujaribu kuingilia kesi hiyo kwa kuwahonga baadhi ya maafisa wa mahakama.

Apoko hata hivyo hivyo alieleza kuridhishwa kwake na jinsi polisi walivyoshiriki sehemu yao katika kesi hiyo.

"Kama kweli nilipigwa hadharani mchana watu wakiona na Alai aweze kudhibiti korti ata heri Wakenya wahame waende nchini zingine. Lakini nataka kushukuru polisi nimeona faili yao iko sawa. Nilikuwa nafikiri kuna vitu vimeibwa lakini iko sawa. Tunangoja mahakama," Alisema Ringtone.

Siku ya Jumatatu mahakama iliahirisha kesi hiyo kwa mara nyingine hadi June 3, 2022. Hata hivyo shahidi mkuu aliweza kutoa ushahidi wake.

Apoko alikuwa ameandamana na wakili wake Evans Ondiek ambaye anaendelea kuuguza majeraha baada ya kuhusika katika ajali.

Mwanamuziki huyo alikuwa amevalia shati yenye matone ya damu na kudai kuwa ni nguo ambayo alikuwa amevalia wakati Alai alimpiga.

"Nilivaa hii Tshati kwa sababu nilikuwa nakuja kutoa ushahidi. Mimi ni msanii. Kwa kuwa nilipigwa damu ikatoka nilitaka hakimu aone mahali damu ilimwagika," Alieleza.

Ringtone na Alai walisababisha kizaazaa mnamo Juni 23 mwaka jana wakati walikabiliana katika barabara moja jijini Nairobi.