Ulinganisho kati ya Tasnia ya Muziki ya Kenya na Tasnia ya Muziki ya Tanzania

Muhtasari

•Hata tunapowashangilia majirani zetu katika Afrika Mashariki,sisi pia tunahitaji kujitahidi kuwa katika nafasi ya kutambulika.

Diamond Platnumz wa Tanzania na Otile Brown wa Kenya ni miongoni mwa wasanii wakubwa zaidi kote Afrika
Diamond Platnumz wa Tanzania na Otile Brown wa Kenya ni miongoni mwa wasanii wakubwa zaidi kote Afrika
Image: INSTAGRAM

Kwa miaka mingi watu wameendelea kulinganisha tasnia ya muziki ya Kenya na ile ya Tanzania. Aghalabu mjadala umeishia kwa Kenya kupata alama ndogo kuliko majirani wetu kwenye upande wa kusini.

Kinachoifanya tasnia ya muziki wa Tanzania kuonekana bora ni suala ambalo sisi kama Wakenya tunapaswa kuliangazia kwa kina.

Hata tunapowashangilia majirani zetu katika Afrika Mashariki,sisi pia tunahitaji kujitahidi kuwa katika nafasi ya kutambulika.

Katika makala haya tutaangazia mambo ambayo yanatofautisha tasnia ya Kenya na Tanzania. Haya ni baadhi ya mambo ambayo yanatofautisha tasnia hizo mbili:-

Uthamini

Suala la kuthaminika kwa wasanii wa Bongo nchini kwao ni jambo ambalo linafanya tasnia yao kubobea. Raia wa Tanzania wanajulikana kuthamini wasanii wao na kushabikia muziki wao kwa kiwango kikubwa tofauti na hapa nchini Kenya ambapo kwa mara kwa mara wasanii wetu wamewashtumu mashabiki na vyombo vya habari kwa kukosa kuthamini muziki wa hapa nchini.

Hili ni suala ambalo mchekeshaji Eric Omondi amekuwa akipigania sana huku akipendekeza muziki wa hapa nchini kuchezwa angalau asilimia 75. Iwapo vyombo vya habari, maeneo ya burudani na mashabiki wataupigia muziki wa Kenya upato zaidi basi nafikiri ni wazi kuwa wasanii wetu watajitahidi zaidi

• Mirabaha

Suala la mirabaha ni suala ambalo wasanii wengi wa Kenya wamekuwa wakilalamika kuhusu. Wasanii wengi wamejitokeza kulalamika kuwa serikali ya Kenya haithamini wasanii wa hapa nchini kama inavyofanyika katika nchi zingine kama Tanzania.

Ingawa pia wasanii wa Bongo wamesikika wakilalamika kuhusu mirabaha yao mara kwa mara, ukweli ni kuwa kitengo kinachosimamia Hakimiliki ya Muziki wao kinawapa zaidi kuliko wanachopata wasanii wa Kenya.

• Kujiuza kwa wasanii

Wasanii wa Bongo wamejifunza sanaa ya kujiuza hadi nje ya mipaka ya nchi yao, jambo ambalo wasanii wa hapa Kenya hawajatilia maanani sana.

Ni wachache tu kati ya wasanii wa Kenya, hasa wasanii chipukizi ambao hutoka nje ya nchi kutumbuiza ama kunadi muziki wao. Wasanii wa Bongo wameweza kuuza muziki wao kote duniani kupitia ziara, matangazo na mitandao ya kijamii na matumbuizo.

•  Ushirikiano

Ingawa suala la wasanii kutoshirikiana limekumba tasnia za nchi nyingi kote duniani, ni wazi kwamba kiwango cha wasanii kutoshirikiana kipo juu nchini Kenya kuliko Tanzania.

Ni vyema wanamuziki kuinuana bila kuoneana kijicho kwani hivyo tu ndivyo tutakavyoweza kukuza muziki wetu.

Lebo

Lebo za kimuziki nchini Tanzania zimeonekana kubobea sana zaidi ya hapa nchini Kenya. Lebo maarufu kama Wasafi na Kondegang zimeweza kusaini wasanii wengi na kukuza talanta zao.

Nchini Kenya hata hivyo, lebo hazijaonekana kufanya kazi sana. Ingawa kunazo lebo kadhaa zinazoendelezwa hapa, sio nyingi ambazo zimeweza kufikia kiwango cha kutambulika nje ya mipaka yetu.