Bahati akubali jina 'Mathew' ambalo alibatizwa na Raila

Muhtasari

•Tukio hilo lilitokea Jumapili katika mkutano mkubwa wa kisiasa uliofanyika katika uwanja wa Kamukunji, jijini Nairobi.

•Mke wa msanii huyo Diana Marua pia ameonekana kukubali jina hilo mpya mumewe alipatiwa na Raila Odinga. 

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Video ya mgombea urais kwa tikiti ya Muungano wa Umoja Raila Odinga akikosea jina la mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Tukio hilo lilitokea Jumapili katika mkutano mkubwa wa kisiasa uliofanyika katika uwanja wa Kamukunji, jijini Nairobi.

Raila alikuwa  anawatambulisha wawaniaji viti mbalimbali waliokuwepo kwenye hafla hiyo lakini hakupata jina la Bahati vizuri alipomwambia.

"Bahati, Mathare," Mwanamuziki huyo alisikika akimwambia kinara wa ODM mara kadhaa ili aweze kulipata.

Hata hivyo Raila hakuweza kupata jina la  mgombea kiti cha ubunge cha Mathare huyo na akaendelea kumtambulisha kama 'Mathew'.

Bila kufahamu kuhusu mchanganyiko uliotokea mgombea urais huyo aliendelea kutambulisha wanasiasa wengine huku akimtambulisha Jalang'o wa Lang'ata baada ya hapo.

Licha ya kejeli chungu nzima ambazo amepokea kwenye mitandao ya kijamii kufuatia tukio hilo, Bahati amechapisha video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuandika ujumbe unaoonyesha akikubali jina hilo mpya.

"Mnasema Baba ameniongezea jina tuu hivyoo.. Bahati Kioko almaarufu Mathew. Nimekubali," Mwanamuziki huyo aliandika.

Mke wa msanii huyo Diana Marua pia ameonekana kukubali jina hilo mpya mumewe alilobatizwa Jumapili.

"Hii imenifurahisha sana. Baba huwa sahihi kila wakati!! MATHEW," Diana aliandika chini ya ujumbe wa mumewe.

Bahati anawania kiti cha ubunge wa Mathare kwa tikiti ya chama cha Jubilee ambacho ni mojawapo wa vyama vilivyounda muungano wa Azimio la Umoja.

Siku kadhaa zilizopita mwanamuziki huyo alikuwa ameonekana kukatizwa tamaa katika azma yake huku akilalamikia kupokonywa tikiti yake ya uteuzi.

Hata hivyo aliweza kupata afueni wiki jana baada ya chama hicho tawala kumrejeshea tikiti yake na kumruhusu awanie kiti.