"Nipo single!" Mama ya Hamisa Mobetto atangaza yupo tayari kuolewa na kijana mdogo

Muhtasari

•Bi Shufaa Lutigunga alisema kuwa yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mengine pindi akitokea mwanaume anayemtaka na ambaye atauridhisha moyo wake.

•Mama Mobetto amesema hakuna sheria wala desturi zinazomzuia kufunga ndoa na mwanaume ambaye ana umri mdogo kuliko yeye.

Image: INSTAGRAM// MAMA MOBETTO

Mama ya mwanamuziki na muigizaji maarufu Hamisa Mobetto ametangaza kuwa ameachika na kwa sasa hana mchumba.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa EP ya bintiye, Bi Shufaa Lutigunga alisema kuwa yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mengine pindi akitokea mwanaume anayemtaka na ambaye atauridhisha moyo wake.

Mama Hamisa aliweka wazi kuwa hatabagua mwanaume yeyote kuhusiana na suala la umri wake, iwe ni mkubwa ama mdogo kuliko yeye.

"Mimi ni single. Nimeachika saa hii niko single. Kama kuna mtu anataka kunioa mimi siwezi kukataa," Bi Lutigunga alisema.

Kumekuwa na tetesi nyingi hasa mitandaoni kuwa Mama Mobetto amekuwa akitoka kimapenzi na vijana wadogo.

Akijibu madai hayo, Mama Mobetto alisema hakuna sheria wala desturi zinazomzuia kufunga ndoa na mwanaume ambaye ana umri mdogo kuliko yeye.

"Mimi ni mwanamke wa Kiislamu. Akitokea mwanaume mdogo na anataka kunioa, Mashallah. Mtume mwenyewe amemuoa Bi Khadija. Bi Khadija alikuwa mkubwa naye mtume alikuwa mdogo. Ikitokea kijana mdogo anataka kunioa mi niko single nimeachika," Alisema.

Aliongeza, "Kijana mdogo akienda kwa mama yangu pale, akasema anataka kuniona na nimeridhika na ananipenda, Mashallah." 

Mama Mobetto hata hivyo alisisitiza kuwa hakuna ushahidi unaomhusisha na kutoka kimapenzi na vijana wadogo.

Bi Lutigunga pia alifichua kuwa kufikia sasa amepokea posa nyingi kutoka kwa wanaume wanaommezea mate binti yake. Alisema ni wanaume wengi ambao wamewahi kufika kwake  wakijaribu bahati yao kwa mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz.

"Kazi yangu ni kupokea posa. Posa nimekula nyingi. Ata leo nimekula posa. Wakati yeye anahojiwa huko mimi nimekula posa," Lutigunga aliambia waandishi wa habari.

Licha ya kuwa wanaume wengi wamewahi kujitokeza kuomba ndoa na Hamisa, mama yake alifichua amekuwa makini sana katika suala la mahusiano yake.