Wajackoyah awaalika Mbusi na Lion kuhudhuria uzinduzi wa Manifesto yake

Muhtasari

•Wajackoyah alisema kuwa Mbusii na Lion ni miongoni mwa wageni wengi ambao wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo.

•Mgombea huyo wa urais kwa mara ya kwanza alifichua kuwa Manifesto yake ina ajenda kuu kumi na mbili.

Image: MAKTABA

Mgombea urais kwa tikiti ya Roots Party of Kenya George Wajackoyah ametangaza kuwa amewaalika watangazaji wa Radio Jambo Mbusii na Lion kwenye uzinduzi wa Manifesto yake.

Akiwa kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen, Wajackoyah  alifichua kuwa atazindua Manifesto yake mnamo Julai 2.

Alisema kuwa watangazaji wa Mbusii na Lion Teketeke ni miongoni mwa wageni wengi ambao wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo.

"Tutazindua Manifesto na tutawafahamisha Wakenya. Tutakuwa na watu kama Mbusii na Lion na marafiki wetu kutoka Yemen watakuja," Wajackoyah alisema.

Mgombea huyo wa urais kwa mara ya kwanza alifichua kuwa Manifesto yake ina ajenda kuu kumi na mbili.

Alifichua kuwa baadhi ya ajenda zake zitakuwa kuhalalisha bangi, kutengeneza ajira na kuboresha uchumi.

"Huu ndio wakati pekee ambao Wakenya wana fursa ya kubadili nchi hii. Kuna wagombea urais wanne na kati ya wanne hao kuna kundi moja tu, mimi na Justina, ambalo linawajali Wakenya kwa kweli,"  Alisema.

Wajackoyah alitoa hakikisho kuwa kampeni zao zitakuwa za amani huku akiapa kuwa hawatupa maneno ya matusi kwa wapinzani wao.

Mgombea mwenza wake Justina Wamae aliwaomba wapinzani wao kukubali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 jinsi tu yatakavyokuwa.

"Rastaman ni mtu wa amani. Tunaambia viongozi wote, Wakenya wasipowapatie nafasi tafadhali rudini kwenye kazi zenu. Mpatieni ambaye atashinda nafasi ya  kufanya kazi zao. Lakini akikuita mfanye kazi pamoja ni sawa, maslahi ya Kenya ni kubwa. Sisi kama Warasta ni watu wenye amani na hamtasikia vurugu zozote kutoka kwetu," Alisema.

Wajackoyah atamenyana na Raila Odinga wa Azimio-One Kenya, William Ruto wa Kenya Kwanza na David Waihiga wa Agano Party.