Mchango wa Uhuru katika msaada wa matibabu ya mwigizaji wa Vioja Mahakamani

Muhtasari
  • Rufaa hiyo ilisema kuwa Gibson alikuwa na mfadhili wa figo lakini anahitaji sh milioni 6 kwa ajili ya kupandikiza figo
Mwigizahi wa Vioja Mahakamani Gibson Gathu
Mwigizahi wa Vioja Mahakamani Gibson Gathu
Image: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta amemnusuru aliyekuwa mwigizaji wa Vioja Mahakamani Gibson Gathu Mbugua.

Gibson, ambaye alipata umaarufu kutokana na jukumu lake kama mwendesha mashtaka katika onyesho hilo, alikuwa akichangisha pesa za kusuluhisha upandikizaji wa figo yake na kuhudumia matibabu ya baada ya upasuaji.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Charter ndani ya jumba la Kaunti ya Nairobi ambapo Rais Kenyatta alituma mchango mkubwa.

“Rais Kenyatta ambaye ni rafiki mkubwa alituma mchango wake wa kibinafsi wa Sh2 milioni. Sisi kama familia na kamati tunamshukuru kwa msaada huo,” mwigizaji huyo alisema.

Bango la msaada wa matibabu lilisoma kwamba figo za Gibson hazikufaulu mnamo 2020 na amekuwa akihudhuria dayalisisi mara mbili kwa wiki.

Rufaa hiyo ilisema kuwa Gibson alikuwa na mfadhili wa figo lakini anahitaji sh milioni 6 kwa ajili ya kupandikiza figo.

Kisha harambee iliratibiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2022 katika Ukumbi wa City, Nairobi, kuanzia saa nane mchana.

Wasamaria wema na mashabiki, waliombwa kutuma michango yao kwa Paybill No: 247247 Account No: 777626 Jina la Akaunti: Gibson Gathu Mbugua.