KRA yaandikisha historia kwa kukusanya zaidi Ksh. trilioni 2

KRA ilikukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.031 katika kipindi cha mwaka wa 2021/22.

Muhtasari

• Kamishna Mkuu wa KRA Githii Mburu alisema mafanikio haya yanatokana na kuboreshwa kwa mikakati ya ukusanyaji kodi na watu wengi pia kuzingatia ulipaji ushuru.

Kamishna jenerali wa KRA, Githii Mburu
Kamishna jenerali wa KRA, Githii Mburu
Image: Maktaba

 Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji ushuru baada ya kuandikisha historia kwa kuvuka kima cha shilingi trilioni 2 katika katika kipindi cha matumizi ya pesa cha mwaka 2021/2022 kutoka shilingi trilioni 1.669 kipindi cha mwaka wa 2020/2021.

Hii ni mara ya kwanza KRA kusajili ushuru wa zaidi ya shilingi trilioni 2 kwa kukusanya jumla  ya shilingi trilioni 2.031 katika kipindi cha mwaka wa 2021/22.

Kamishna Mkuu wa KRA Githii Mburu alisema mafanikio haya yanatokana na kuboreshwa kwa mikakati ya ukusanyaji kodi na watu wengi pia kuzingatia ulipaji ushuru.

Githii alisema walikusanya ushuru wa ndani wa jumla ya shilingi trilioni 1.297 dhidi ya lengo la shilingi trilioni 1.267 huku idara ya Forodha na Mipaka ikikusanya jumla ya shilingi bilioni 728.530 dhidi ya lengo lililowekwa la shilingi bilioni 702.823.

"Ukusanyaji wa mapato wa shilingi trilioni 2.031 unaashiria kiwango cha juu cha ushuru uliokusanywa," alisema.

Githii alionegeza kuwa..."Huu ndio ukuaji wa juu zaidi wa mapato katika historia ya KRA."