(Video) "Nakupenda sana!" Kajala aweka bango kubwa barabarani kumsherehekea bintiye Paula

"Kheri za siku ya kuzaliwa Paula. Mama anakupenda," Bango lilisoma

Muhtasari

•Paula  ambaye ni bintiye muigizaji Fridah Kajala Masanja  na mtayarishaji wa muziki P-Funk Majani ametimiza miaka 20.

•"Nyie nyie nyie jamani mna mama kama wangu jamani.. nyie jamani Kajala Frida," Paula alipongeza juhudi za mamake.

Paula Kajala na mamake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// PAULA PAUL KAJALA

Hivi leo (Julai 15) mwanamitindo wa Tanzania, Paula Paul Kajala anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Paula  ambaye ni bintiye muigizaji Fridah Kajala Masanja  na mtayarishaji wa muziki P-Funk Majani ametimiza miaka 20.

Wanamitandao, marafiki, mashabiki na watu wengine wa karibu wameendelea kumsherehekea kipusa huyo anapoingia kwenye hatua mpya.

Mamake Paula hata hivyo ndiye alijitokeza zaidi kwa kuweka bango kubwa lenye picha yake kando ya barabara.

Kajala ambaye kwa sasa yupo nchini Qatar kwa ziara ya kikazi alifanya bango lenye picha ya bintiye na maandishi  ya kumsherehekea kuwekwa kando ya barabara iliyo katika eneo la Posta nchini Tanzania.

"Kheri za siku ya kuzaliwa Paula. Mama anakupenda," Maandishi ya bango hilo yalisoma.

Marafiki wake Paula ndio waliompeleka hadi katika eneo ambalo  bango limewekwa mwendo wa usiku wa manane.

Katika kipindi chote cha safari ya kutoka Mbezi hadi Posta, Paula alionekana kutofahamu ambacho marafiki zake walikusudia kufanya na alisisimka mno punde baada ya kuona bango alilowekewa.  Hilo lilimpata kama surprise.

"Asante kwa mama yangu na baba. Nawapenda. Angalieni jameni, mnaniona," Paula alisikika akisema katika kanda ya video aliyopakia Instagram. 

Katika video hiyo bintiye Kajala alionekana mchangamfu mno na hata kushindwa kuzuia furaha yake kubwa.

"Nyie nyie nyie jamani mna mama kama wangu jamani.. nyie jamani Kajala Frida," Paula alipongeza juhudi za mamake.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Kajala alimhakikishia bintiye kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Nakupenda sana na nakumiss," Mchumba huyo wa Harmonize alisema

Hatua ya Kajala kuweka bango inajiri miezi michache tu baada ya mchumba wake Harmonize kupiga hatua kama hiyo.

Harmonize hata hivyo alifanya vile mwezi Machi katika juhudi ya kuomba msamaha na kurejesha mahusiona yao yaliyokuwa yamekatika mwaka jana.

Akizungumza katika mahojiano ya awali alifichua kwamba  bango hilo lenye maandishi 'Lovers' aliloweka katika eneo la Kinondoni lilimgharimu shilingi milioni 12  za Tanzania. (Ksh 600,000)

"Niliweka mimi 100%. Nilitumia milioni 12. Itakuwa pale kwa takriban miezi sita," Harmonize alisema.

Juhudi za bosi huyo zililipa kwani baadae Kajala alimsamehe na wakarudiana. Wawili hao tayari wanapanga ndoa baada ya Harmonize kumvisha muigizaji huyo pete ya uchumba.