Njugush asimulia kisa cha kuvunja moyo kuhusu ukatili kazini

Njugush amewakashifu mabosi wakatili na kuwaonya kuwa maovu yao yatawageukia siku moja.

Muhtasari

•Njugush amesimulia kisa cha kusikitisha cha tukio ambalo alishuhudia katika eneo moja la burudani huko Kamakis.

•Njugush amesema kuwa inasikitisha sana kuona mambo magumu ambayo watu wanaohangaika kukidhi mahitaji yao ya msingi wanapitia.

Image: INSTAGRAM// BLESSED NJUGUSH

Mchekeshaji Timothy Kimani almaarufu Njugush amewasuta mabosi ambao huwa wakatili kwa  wafanyikazi wao.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Njugush amesimulia kisa cha kuvunja moyo cha tukio ambalo alishuhudia katika eneo moja la burudani huko Kamakis.

Njugush alisimulia jinsi alipokuwa akifurahia nyama choma  yake alijitokeza mwanaume mmoja mfupi na kuanza kumnyanyasa mhudumu mdogo kwa sababu ya kuchelewa chakula alichokuwa ameagizwa.

Alisema mwanaume huyo ambaye baadae alibaini kuwa ni meneja katika mkahawa huo  alimvuruta mhudumu yule hadi mahali fiche na kuanza kumzaba makofi

"Kwa muda nadhani wanacheza tu. Alimvuta yule jamaa nyuma ya mlango ulioandikwa "Wafanyakazi tu" makofi yakaanza kulia ,katika hatua nikajua ni mbaya. Hakufikiria  kuna mtu yeyote anaona anachofanya. Hivyo kijana akajinasua na kuja katika mwanga, aalama za vidole zikionekana wazi kwenye shavu lake," Alisimulia Njugush.

Baada ya mhudumu huyo kujinasua , meneja alifuata nyuma na kuwageukia wafanyikazi wengine huku akitishia  kuwafuta kazi na kuleta wahudumu wapya.

"Siwezi kuamini bana. Wote walikuwa na hofu machoni, walitokwa na damu kutoka ndani!" Njugush alisema.

Mambo yaliendelea kumharibikia mhudumu yule kwani meneja anaripotiwa kutamatisha kazi yake katika mkahawa huo mara moja.

Njugush amesema kuwa inasikitisha sana kuona mambo magumu ambayo watu wanaohangaika kukidhi mahitaji yao ya msingi wanapitia.

"Lakini Mungu anajua watu wanapitia nini kuweka chakula mezani. Mungu halali atawakumbuka," Aliandika.

Mchekeshaji huyo aliwakashifu mabosi wakatili na kuwaonya kuwa maovu yao yatakuja kuwageukia siku moja.

"Kwa wale miungu wadogo ambao wanadhani wengine ni watoto wa mungu mdogo, mtalipa, ikiwa sio, watoto wenu watalipa!" Alisema Njugush.

Wanamitandao waliosoma chapisho hilo la Njugush walitoa hisia mseto huku wengi wakilaani kitendo cha meneja huyo.