Mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefunguka kuhusu maendeleo ya ujauzito wa mkewe Diana Marua.
Akiwahutubia mashabiki wake katika tamasha la Wamusyi Night lililofanyika wikendi, baba mzazi huyo wa watoto watatu alifichua kuwa tarehe ya kujifungua ya mke wake iko imekaribia sana sasa.
"Diana anatarajia kujifungua dakika yoyote sasa!" Bahati alitangaza.
Mwimbaji huyo alibainisha kuwa sasa anakaa karibu na mkewe mara nyingi kwa sababu anaweza kupata uchungu wa leba wakati wowote.
"Lazima nikae karibu na nyumbani," alisema.
Wanandoa hao ambao wamekuwa pamoja kwa takriban miaka sita wanatarajia mtoto wao wa tatu pamoja. Tayari wana mtoto mmoja wa kike na mwingine wa kiume pamoja, Heaven Bahati na Majesty Bahati.
Bahati hata hivyo ana mtoto mwingine mmoja na aliyekuwa mpenzi wake, Yvette Obura.
Mueni Bahati ambaye ni mtoto wa kwanza wa Bahati alizaliwa kabla ya mwimbaji huyo kujitosa kwenye mahusiano na Diana. Kwa sasa msanii huyo anashirikiana vizuri na Bahati katika malezi ya binti yao.
Bahati na Diana walitangaza ujauzito wa mtoto wao wa tatu takriban miezi mitatu iliyopita kupitia wimbo 'Nakulombotov.' Diana aliufichua ujauzito wake mkubwa katika video ya wimbo huo ambao alishirikiana na mume wake.
Katika wimbo huo wa dakika tatu wanandoa hao walitoa ahadi kemkem na ushauri kwa mtoto wao ambaye hajazaliwa. Wawili hao pia walimhakishia mtoto wao kuhusu upendo wao mkubwa kwake na kumtakia baraka tele maishani.
"Nakutakia baraka, nakutakia fanaka,
Nakutolea sadaka, nyota yako itawaka,
Utamkia neema isiyokuwa na mipaka.
Maisha mazuri, uishi mamiaka.
Magonjwa na mikosi na zikae mbali,
Malaika wakulinde dhidi ya ajali.
Hekima ikutawale kama serikali,
Nasi tunakusubiri kama fainali," Diana alisema katika kipande cha wimbo huo.
Rapa huyo pia alimfahamisha mtoto wake kuhusu jinsi dunia ilivyo huku akimueleza kuwa kwa kawaida mambo sio rahisi.
Siku chache zilizopita wanandoa hao walizua wasiwasi mkubwa miongoni mwa mashabiki wao baada ya Diana kuchapisha ujumbe wa kutia wasiwasi huku Bahati akifuta machapisho yote kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Wasiwashi huo hata hivyo ulifutwa baada ya Bahati kuachia kibao chake cha kwanza baada ya muda mrefu. Wimbo 'Mambo ya Mhesh' ulikuwa wake wa kwanza tangu kupoteza kinyang'anyiro cha ubunge wa Mathare mwezi Agosti.