Ni maarufu pia! Butita afunguka kuhusu mpenzi wake mjamzito

Mchekeshaji huyo alidokeza kuwa mpenzi wake ni muigizaji maarufu.

Muhtasari

• Butita alibainisha kuwa hayupo tayari kumfichua mpenzi wake hadharani na kudai kuwa wanamitandao wana mazoea ya kuvunja ndoa za watu.

•Alifichua kwamba kuna mipango ya yeye na mpenziwe kufanya karamu ya kufichua jinsia ya mtoto wanayetarajia 

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Eddie Butita

Mchekeshaji Eddie Butita amefichua kuwa mpenzi wake ambaye alimtangaza kuwa mja mzito siku ya Alhamisi ni mtu maarufu.

Katika mahojiano yake na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, alibainisha kuwa hayupo tayari kumfichua mpenzi wake hadharani na kudai kuwa wanamitandao wana mazoea ya kuvunja ndoa za watu.

Butita hata hivyo alidokeza kuwa mpenzi wake ni muigizaji.

"Sasa shemeji yetu ni nani?" aliulizwa.

Alijibu, "Ni mke wangu huyo, si mpenzi wangu. Siwezi wapa mabinti wa watu ujauzito, hiyo ni tabia gani? Ni mtu maarufu kivyake ambaye amekuwa kwenye tasnia ya burudani, si mwanamuziki wala mchekeshaji. Na pia si mwanasiasa."

Alifichua kwamba kuna mipango ya yeye na mpenziwe kufanya karamu ya kufichua jinsia ya mtoto wanayetarajia Jumatatu wiki ijayo.

Aliongeza kuwa tafrija hiyo ya kifahari itafanywa katika hoteli moja ambayo alisita kufichua kwa kuwa itakuwa hafla ya faragha.

"Sitawaambia ni hoteli gani kwa kuwa sitaki watu wengi ,ni ya waalikwa pekee na nimealika watu sita tu, wanasiasa wawili na marafiki wa karibu wanne,"  alisema.

Alifichua kuwa mpenzi wake amekuwa mjamzito kwa takriban miezi saba sasa na wamekuwa kwenye mahusiano kwa muda huo.

Mchekeshaji huyo hakufichua hata jina wala maelezo ya kibinafsi ya mpenzi wake ila alifichua kuwa jina lake lina herufi A.

Butita alitangaza kuwa yeye na mpenzi wake ambaye bado hajajulikana wanatarajia mtoto siku ya  Alhamisi.

Kwenye Instagram, alipakia video iliyoonyesha akipapasa ujauzito wa mpenziwe huku wimbo wa Nadia na ArrowBoy 'Kai' ukicheza kwa umbali.

Alieleza jinsi anavyotamani kujua jinsia ya mtoto wake.

"Hakuna maneno yanayoweza kutumika kueleza hili. Nambari 2 imekuwa nambari yangu ya bahati na 2022 ina 2 tatu. Ni mtoto wa kike au wa kiume? Tuonane Jumatatu,"  aliandika.