"Nimetumwa na Mungu!" Msanii kutoka Kakamega ataka kuolewa na mbunge Salasya

Malesi alisema yeye ni wife material ambaye anaelewa maana ya kuwa mke wa mtu.

Muhtasari

•Juliana alisema baada ya kusali na kufunga ili kufunuliwa ni nani ambaye Mungu alimtaka afunge ndoa naye, roho yake ilimwelekeza kwa mbunge huyo wa muhula wa kwanza.

•“Nitamuonyesha mapenzi ambayo hajawahi kukutana nayo tangu azaliwe,” alisema Juliana.

mwenye umri wa miaka 28 anasema Mungu alimfunulia kuwa mbunge Peter Salasya ni mume wake
Msanii wa nyimbo za Injili Juliana Kadogo mwenye umri wa miaka 28 anasema Mungu alimfunulia kuwa mbunge Peter Salasya ni mume wake
Image: DAVID MUSUNDI

Mwanamuziki kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya Juliana Malesi Kakai amesema kuwa yeye ndiye chaguo bora la mwenzi kwa Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya.

Akizungumza mjini Kitale siku ya Jumatano, Juliana alisema baada ya kusali na kufunga ili kufunuliwa ni nani ambaye Mungu alimtaka afunge ndoa naye, roho yake ilimwelekeza kwa mbunge huyo wa muhula wa kwanza.

“Nimeamua na sasa niko tayari kuolewa na Peter Salasya, mwanamume ninayeamini rohoni mwangu ndiye mume wangu niliyepewa na Mungu,” msanii huyo mwenye umri wa miaka 28 alisema.

"Nimeamua kwamba nitaolewa na Peter Salasya, mwanamume anayeupendeza moyo wangu na katika mpango wa Mungu," alisema.

Alisema hafai kukashifiwa na mtu yeyote kwa kumuomba mbunge huyo amuoe kwa sababu alijitangaza kuwa yupo single na anataka mwanamke mzuri na mrembo wa kuoa.

 “Nilimuona mbunge akivuma kwenye mitandao ya kijamii kuwa anatafuta mke. Kama mwanamke kutoka Koyonzo katika eneo bunge jirani la Matungu, nilisema wacha nitafute msaada wa Mungu na Mungu amenileta hapa kusema ninachosema sasa," alisema.

Malesi alisema yeye ni wife material ambaye anaelewa maana ya kuwa mke wa mtu.

“Nitamuonyesha mapenzi ambayo hajawahi kukutana nayo tangu azaliwe,” alisema Malesi.

Juliana ameimba nyimbo kadhaa ambazo ni pamoja na khukhonyane ( tusaidiane).

Alipoulizwa  kama anavutiwa na mbunge huyo kwa muhula wa kwanza kwa sababu ya pesa, alikanusha.

"Ningekubali kuolewa kitambo na wanaume matajiri wenye pesa nyingi zaidi. Sauti  ya Mungu imesema nitaolewa na Peter Salasya hasa," alisimulia.

Utafsiri: Samuel Maina