Staa wa bongo Harmonize amejibu madai kwamba alipakia video ya wimbo wa albamu yake mpya akiwa na mpenzi wake wa zamani Briana.
Harmonize alipuuzilia mbali madai hayo na kusema kuwa video hiyo ilikuwa ya kitambo, si ya hivi majuzi.
Video iliyoachiwa ni ya wimbo wake wa 'The Way You Are'.
"Ni video ya kitambo, iliachiwa kimakosa. Timu yangu inashughulikia jambo hilo. Mwanaume mnene aliye kwenye video hiyo sio mimi," Harmonize alisema.
Msanii huyo alimsifia mchumba wake Kajala kwa kuhakikisha kuwa ana mabadiliko katika umbo lake.
"Mwili wangu una afadhali, mke wangu alinifanyia jambo, asante mpenzi wangu.Hakuna ninaloweza kufanya kuhusu mambo ya zamani,"aliongeza.
Hata hivyo, msanii huyo aliwakejeli wapenzi wake watatu wa zamani akiwemo Briana katika wimbo wake wa 'My Way'.
Katika wimbo huo Harmonize aliwashambulia wapenzi wake watatu wa zamani,Wolper, Sarah na Briana na kumsifia mchumba wake wa sasa Kajala Masanja.
Alidokeza kuwa bado alikuwa mgeni wa mapenzi wakati akichumbiana na Wolper na alitengana naye kufuatia hofu ya kushindana na mabwenyenye.
"Ile mwanzo mwanzo nalijua kopa, moyo ukadondoka kwa Wolper. Ningali bado mdogo nikaogopa, Hivi nitawezaje kushindana na vibopa," alisema Harmonize katika kifungu cha Wimbo huo wa dakika mbili.
Aliendelea kuzipuuza pesa za mwanamitindo Sarah Michelloti ambaye alichumbiana naye kwa muda na kusema ni karatasi tu.
"Nikasema hasara roho pesa makaratasi , si nikampa Sarah roho kulipiza kisasi. Labda niseme ni mambo ya ujana, ama pengine nyota zilipishana. Kila siku tukawa tunagombana, hapa kati kabla hajaja Briana," aliimba.