"Nimeteseka!" Mwanahabari wa 'Why are you gay?' avunja kimya kuhusu mahojiano yake yaliyovuma

Lakini kusema kweli, hii ilikuwa miaka kumi iliyopita! Boy child ameteseka. " Kaggwa alisema.

Muhtasari

•Katika mahojiano hayo, Kaggwa alionekana kukerwa na sababu ya mwanaharakati huyo kuchagua kuwa shoga na alitaka sana kuelewa yeye ni nani hasa.

•Jibu la mwanahabari huyo linadokeza kwamba mahojiano hayo huenda yalimletea matatizo fulaniyasiyojulikana.

Image: TWITTER// SIMON KAGGWA NJALA

Mwanahabari wa Uganda Simon Kaggwa Njala ameonekana kuchoshwa na watu kufufua kumbukumbu za mahojiano maarufu aliyofanya muongo mmoja uliopita.

Miaka kadhaa iliyopita Bw Kaggwa alimkaribisha mwanaharakati wa haki za binadamu wa Uganda Pepe Julian Onziema katika kipindi chake cha Morning Breeze kwenye runinga ya NBS ambapo walikuwa na mahojiano ya wazi kuhusu ushoga nchini Uganda.

Katika mahojiano hayo, Kaggwa alionekana kukerwa na sababu ya mwanaharakati huyo kuchagua kuwa shoga na alitaka sana kuelewa yeye ni nani hasa.

"Why are you gay? (Kwa nini wewe ni shoga)?" Kaggwa aliuliza mara kwa mara huku mahojiano yakiendelea.

Onziema ambaye alizaliwa mwanamke hata hivyo hakutaka kuitwa shoga na kusisitiza kuwa yeye ni mwanamume anayevutiwa na wanamke.

"Mimi si mwanaharakati wa haki za binadamu anayetetea usawa kwa watu wenye mtazamo tofauti wa kimapenzi na ujinsia tofauti," alisema.

Onziema pia alikiri kuwa na mpenzi mwanamke lakini akaweka wazi kuwa hakuwa akishiriki tendo la ndoa naye.

Alipuuzilia mbali madai kwamba alikuwa akipigia debe ushoga nchini Uganda na akakana kuwa alilipwa kufanya hivyo.

Mahojiano hayo magumu yalikuwa yakiendelea vizuri kabla ya Mchungaji Martin Ssempa ,ambaye ni mkosoaji mkubwa wa wapenzi wa jinsia moja, kuingia studio na kulaani mienendo ya Onziema. Punde baada ya kumuona Bw Ssemoa, mwanaharakati huyo  alisimama na kutoka nje lakini alishawishiwa na kurudi  baada ya muda mfupi.

Mahojiano hayo ya zaidi ya saa moja yamekuwa gumzo kwenye mitandao kwa takriban miaka mitatu iliyopita huku wanamitandao wakiyarejesha mara kwa mara. 

Hivi majuzi, akaunti ya Twitter @AfricaFactsZone ilichapisha klipu fupi ya mahojiano hayo na kuyataja kama mahojiano maarufu zaidi nchini Uganda.

"Mahojiano maarufu zaidi nchini Uganda. Mwandishi wa habari anauliza mtu kuhusu jinsia yake," maelezo ya video hiyo yalisoma.

Kaggwa ambaye alionekana kuchoshwa na video hiyo kuzungumziwa mara kwa mara alijibu, "Lakini kusema kweli, hii ilikuwa miaka kumi iliyopita! Boy child  ameteseka. "

Jibu la mwanahabari huyo linadokeza kwamba mahojiano hayo huenda yalimletea matatizo fulaniyasiyojulikana.