Tamasha la Kitamaduni la Kila mwaka Lamu kuanza Alhamisi

Tamasha hilo linasemekana kuwa moja ya tamasha maarufu zaidi za Utamaduni duniani.

Muhtasari

• Kila mwaka Lamu huwa hai wakati wa Tamasha la Utamaduni la Lamu, Wakenya wanapokusanyika ili kusherehekea utamaduni, imani na mila.

Gavana wa Lamu Issa Timamy
Gavana wa Lamu Issa Timamy
Image: ANC PARTY/TWITTER

Kisiwa cha Lamu kilicho katika Kaunti ya Lamu, Pwani ya Kenya kinatarajiwa kufanya Tamasha la 20 la Kitamaduni la Kila Mwaka kuanzia Alhamisi hii tarehe 24 Novemba, 2022.

Tamasha hilo linasemekana kuwa moja ya tamasha maarufu zaidi za Utamaduni duniani zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni kulingana na mwandalizi, Gavana wa Lamu Issa Timamy.

“Ningependa kuchukua fursa hii kuwaalika Wakenya kutoka sehemu zote za Jamhuri na raia kutoka mataifa mengine kwa ajili ya tamasha la kitamaduni la siku 3 kwa kuwa hili litakuwa tamasha la aina yake na tuna shughuli kadhaa ambazo zitafanywa baharini na shughuli zingine za kitamaduni ambazo zitavutia maelfu ya watalii wa ndani na nje”, Alisema Issa Timamy.

Gavana wa Lamu ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ANC siku ya Jumanne alisema utawala wake umejitolea kukuza amani, umoja na utangamano kupitia kuimarisha Sekta ya Utamaduni ya Lamu na kuangazia urithi wa kitamaduni wa raia wa Lamu kwa taifa zima na ulimwengu.

Tamasha la Utamaduni la Lamu la mwaka huu lina mada "Kusherehekea utofuati wetu" na Gavana Timamy anasema ni wakati ambao utasaidia kuelewa kuwa na nchi yenye makabila mengi ni nguvu na sio udhaifu.

"Ikiwa  watu watakuja na sisi kuonyesha tamaduni hizi zote mbalimbali na vipaji vya makabila yote yanayoishi Lamu kwa amani basi hii itakuwa ishara kwamba kukusanyika pamoja kama watu ni ishara ya umoja na nguvu katika utofauti." Alisema Issa Timamy kwenye Mahojiano.

“Wanawake wa Lamu wanajulikana kuwa wapishi wazuri na tunataka wageni wetu wapate chakula kitamu kilichotayarishwa na wanawake wa Lamu wakati wa tamasha hili la kitamaduni. Ni wakati wa kujifurahisha, kutafakari na kustarehe,” aliongeza Timamy.

Jamii ya Lamu inafahamika kwa utulivu wake na amani, lakini Tamasha la Utamaduni linapowadia kila mtu anakuwa katika harakati za kufanya mambo haraka. 

Ili kuhimiza uvumilivu wa kitamaduni na vile vile kufurahia, mashindano kadhaa huandaliwa. Kwanza kabisa, tuna mbio za punda ambazo hufanyika na ni shindano ambalo husubiriwa sana kati ya mashindano mengine mengi ambayo hufanyika. Mshindi huishi kwa majivuno mwaka mzima.

Kisha, mbio za jadi za mashua hupangwa na riadha kando mwa bahari na shughuli zingine kuonyesha ushupavu wa wenyeji. Mashindano ya mashua yanatumiwa kuhifadhi na kuhimiza sanaa ya mashua.”

Zaidi ya hayo, tamasha hilo linajumuisha ukaririaji wa mashairi, maonyesho ya muziki na kucheza bao, ambao ni mchezo wa kale zaidi unaojulikana katika historia ya binadamu.

"Tutakuwa na maonyesho ya muziki kutoka mbali hadi Tanzania, tutakuwa na wasanii wetu kutoka Kenya na wasanii wa Ndani kutoka Lamu ambao wataburudisha wageni wetu wakati huu wa tamasha." Alisema Timamy.

Pia tutakuwa na ushairi wa jadi wa Kiswahili, uchoraji wa Henna na shindano la Bao pengine mchezo mkongwe zaidi katika historia ya binadamu, huku ushahidi wa kiakiolojia ukionyesha kwamba mchezo huo umechezwa kwa maelfu ya miaka kote barani Afrika na Mashariki ya Kati.” aliongeza Timamy.

Kila mwaka Lamu huwa hai wakati wa Tamasha la Utamaduni la Lamu, Wakenya wanapokusanyika ili kusherehekea utamaduni, imani na mila ambazo ni moyo na roho ya jamii hii katika kisiwa cha kupendeza cha Lamu.

Kitongoji cha kale cha Waswahili, Lamu ni turathi  ya Urithi wa Dunia na tamasha la kitamaduni hutoa ufahamu wa jinsi maisha ya zamani yalivyokuwa katika masuala ya usanifu na mtindo wa maisha.