Bahati, mpenzi wake wa zamani Yvette Obura wamsherehekea binti yao Mueni

Bahati pia alimhakikishia bintiye kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Muhtasari

•Mueni Bahati anasherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, Novemba 29.

•Bahati alimwarifu binti huyo wake amwambie zawadi ya siku ya kuzaliwa aitakayo na akaahidi kutimiza ombi lake

Mueni Bahati
Image: INSTAGRAM// YVETTE OBURA

Binti ya mwanamuziki Bahati na mpenzi wake wa zamani Yvette Obura, Mueni Bahati anasherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, Novemba 29.

Mueni ambaye kwa sasa anaishi na mama yake Yvette ametimiza miaka 7.

Bahati ambaye hivi majuzi alimkaribisha duniani mtoto wake wa nne amechukua fursa hiyo kumsherehekea mtoto huyo wake wa kwanza na kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa. 

Katika ujumbe ambao alichapisha Instagram, Bahati pia alimhakikishia bintiye kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Binti yangu unapotimiza miaka 7 Leo ningependa nikukumbushe mambo matatu;  Unapendwa na kuthaminiwa na nitakuwa nawe milele, siku zote kumbuka utakuwa na nafasi ya pekee moyoni mwangu kila wakati (Kwangu wewe ni kitu kisichoweza kubadilishwa) na unaweza kunitegemea kila wakati na moja ya sababu ya mimi kufanya kazi kwa bidii leo ni kukupa maisha bora ya kesho," Bahati alimwandikia bintiye.

Mwimbaji huyo pia alimwarifu binti huyo wake amwambie zawadi ya siku ya kuzaliwa aitakayo na akaahidi kutimiza ombi lake.

"Kheri ya kuzaliwa malkia wangu @mueni_bahati, niambie tu zawadi moja ya siku ya kuzaliwa  ambayo unataka na nitakununulia," alimwambia.

Yvette pia alimsherehekea binti yake na kumtaja kama mtoto mrembo, mwerevu, anayependa na mzuri.

"Kheri ya siku ya  kuzaliwa kwa mtu ambaye aliamua kuniweka kwenye leba kwa masaa mengi na hata nikalia juu yake kwa miezi! 🤧🤧❤❤," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Yvette aliambatanisha ujumbe huo na video ya mkusanyiko wa kumbukumbu zake kadhaa na binti huyo wake.

"Nikikuambia safari hii haijakuwa rahisi, weeee lakini Mungu ni nani ?? Pamoja na yote yaliyosemwa na kufanyika, pamoja na kila kitu nilichotupiwa, wewe bado mtoto wangu MUENI,"

"Nakupenda kuliko chochote mpenzi wangu," alisema