"Endeleeni kutuombea!" Nadia Mukami awaomba Wakenya huku akiomboleza

Nadia alitangaza kifo cha mjomba wake Alhamisi na kufichua alifariki wiki iliyopita.

Muhtasari

•"Tulimpoteza mjomba Peter wiki jana. Kaka ya baba yangu. Roho yake ipumzike katika amani nzuri," alisema.

•Nadia alitumia picha hiyo kuwaonyesha wafuasi wake jinsi alivyotoka mbali kufikia mahala ambapo amefika sasa.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa Kenya, Nadia Mukami amemuomboleza mjomba wake, Peter.

Mwimbaji huyo alitangaza kifo cha kaka huyo wa baba yake siku ya Alhamisi na kufichua kwamba alifariki wiki iliyopita.

"Tulimpoteza mjomba Peter wiki jana. Kaka ya baba yangu. Roho yake ipumzike katika amani nzuri," alisema kwenye Instagram.

Katika ujumbe wake, mama huyo wa mtoto mmoja alitoa ombi kwa mashabiki wake kukumbuka familia yao katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza.

"Mungu aipe nguvu familia yetu katika kipindi hiki kigumu, endeleeni kutuombea," aliandika na kuambatanisha na picha ya marehemu mjomba wake.

Pia alichapisha picha nyingine ya kumbukumbu na mjomba huyo wake ambayo ilipigwa siku za utotoni wake.

Nadia alitumia picha hiyo kuwaonyesha wafuasi wake jinsi alivyotoka mbali kufikia mahala ambapo amefika sasa.

"Nione na marehemu mjomba Peter. Apumzike kwa amani! Ukiona nimeshinda unifurahie tu, nimetoka mbali," alisema.

Mwanamuziki huyo ambaye alizaliwa jijini Nairobi ana asili ya Embu ambako alikulia sehemu ya maisha yake.

Mwezi Aprili 2021, Nadia na mzazi mwenza wake Arrow Bwoy walipoteza mtoto wao bado akiwa tumboni.

Alisema alikumbwa na kiwewe kikubwa kutokana na tukio hilo  hadi kulazimika kupata ushauri wa kisaikolojia.

"Ulikuwa wakati mgumu kuwahi pitia. Huo ndio wakati nilitamani singekuwa msanii. Hospitalini nilioshwa, nilipotoka bado nilikuwa na trauma.

Nilipitia kiwewe hadi nikaenda kupata ushauri. Nilikuwa naenda kupata ushauri na watu hawakujua, huo ndio wakati nilikuwa natengeneza ofisi yangu. Nilishauriwa sana na ilisaidia sana," Nadia alisimulia.

Katika kipindi hicho, mama huyo wa mtoto mmoja alijaribu sana kuficha hisia zake na kujifanya kama kwamba yupo sawa.

"Kila mtu alikuwa ananiangalia kama kielelezo, hakuna aliyejali matatizo yangu. Hiyo ndio sababu nilijichagua mimi. Nimeamua kuwa mkweli kadri iwezekanavyo. .. nimepigana sana mwaka uliopita (2021). Kama kuna mtu amejua kujiekelea vitu ni mimi. Nilipoteza marafiki wengi 2021 kwa sababu sikuwa na wakati wa kujieleza," Alisema.

Msanii huyo hata hivyo alibahatika kupata ujauzito mwingine takriban miezi miwili baada ya kupoteza ule wa kwanza. Alijifungua mtoto wa kiume mnamo Machi 4.