Marioo akimbilia Davido kwa msaada baada ya Diamond kumkwepa

Marioo alisema kuwa Davido ndiye atakaye msaidia kutimiza ndoto yake ya kutumbuiza kwenye ukumbi wa O2 Arena nchini UK.

Muhtasari

• Naamini kuwa ntatumbuiza katika Arena 02 jijini London mwaka huu - Marioo.

• Wanamuziki maarufu kutoka nchi ya Nigeria wameweza kutumbuiza katika ukumbi huo ambao ni ndoto ya kila msanii wa Kiafrika.

Staa wa Bongo Omary Mwanga almaarufu Marioo ameweza ameweka wazi lengo lake kuu mwaka huu - kufanya shoo pamoja na msanii nguli wa shughuli hizo kutoka Nigeria Davido.

Marioo alisema kuwa ndoto yake itatimia kama watapanda jukwaani pamoja na Davido na si katika ukumbi wowote tu bali ukumbi uwe ni ule wa O2 Arena wa nchini Uingereza ambao ni ndoto ya kila msanii wa Kiafrika.

"Naamini kuwa nitatumbuiza katika Arena 02 jijini London mwaka huu. Nina uhakika kuwa ndugu yangu Davido atafanya hili liwezekane," alisema Marioo.

Wanamuziki maarufu kutoka nchi ya Nigeria wameweza kutumbuiza katika ukumbi huu wa kihistoria wakiwemo Wizkid, Davido, Tiwa Savage, Burna Boy, D'bnaj, 2baba miongoni mwa majina mengine mengi tajika.

Wizkid alikuwa mwanamuziki wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika Ukumbi huo tarehe  25 ‚Mei 2018 - ukumbi ambao umetumiwa na wasanii mibabe kama vile  Beyonce‚Adele,  Drake miongoni mwa wengine.

Kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, bado hakuna msanii ameweza kufanikisah kuandaa shoo yake kwenye ukumbi huo japo mwaka jana mwezi Septemba kulikuwa na taarifa kwamba msanii namba moja wa muda wote kutoka Afrika Mashariki Diamond Platnumz alikuwa anatarajiwa kutumbuiza kwenye O2 Arena - uvumi ambao ulififia kama moto wa karatasi hata hivyo.

 

Kauli ya Marioo kutegemea Davido kufanikisha ndoto yake ya kufika O2 Arena imetajwa na wakereketwa katika tasnia ya sanaa kuwa ni njia moja ya kufuata kivuli cha Diamond ambaye kabla afanikiwe alipitia mikononi mwa Davido aliyempa shavu kwa remix ya ngoma yake ya 'Number One' - ngoma iliyotoka 2014 na kumtambulisha Diamond kama msanii haswa kule Afrika Magharibi ambako hakuwa anajulikana kabla ya hapo.

Mahusiano baina ya Diamond na Marioo hayajakuwa mazuri hivi majuzi haswa baada ya sekeseke kuwa Marioo aliwahi kumfuata Diamond kinyemela akimtaka kumpa mkataba kama msanii chini ya mwavuli wa WCB Wasafi.

Diamond alifichua haya wiki tatu zilizopita kupitia mahojiano ya kipekee na kituo cha redio cha Wasafi, madai ambayo hata hivyo Marioo alijitokeza na kuyakana bayana akisema, "Ni uongo, mkubwa kateleza mfupa hauna ulimi."

Baadae Marioo katika shoo yake ya 'The Kid You Know' alimpa Diamond mwaliko wa kuhudhuria shoo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Milimani City lakini Diamond hakutokea wala kutuma mwakilishi yeyote, licha ya hapo awali kutokea kweney shoo kama hizo zikiwemo ile ya msanii Barnaba Classic na Juma Jux ambao wote walikuwa wanazindua albamu zao.

Yote tisa, kumi ni kwamba kila mmoja anasubiri kwa hamu kuu kuona iwapo Davido atampa shavu kama alivyofanya kwa Diamond ama naye atamkwepa.