"Wueh!" Bintiye Betty Kyallo, Ivanna ashtushwa na umri wa mama yake

Betty Kyallo atakuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 34 katikati mwa mwezi ujao.

Muhtasari

•Ivanna ambaye ni mtoto wa pekee wa Betty alimuuliza kuhusu umri wake na alionekana kushtushwa sana na jibu yake.

•Mfanyibiashara huyo wa nywele na urembo alimuomba binti huyo wake kwa utani aache kumuaibisha.

Ivanna na mama yake Betty Kyallo
Image: INSTAGRAM// IVANNA

Binti wa mfanyibiashara na mtangazaji mashuhuri Betty Kyallo, Ivanna alionekana kushangaa baada ya kujua umri ambao mama yake atakuwa anatimiza mwaka huu.

Katika video iliyochapishwa kwenye Instagram, Ivanna ambaye ni mtoto wa pekee wa Betty alimuuliza kuhusu umri wake na alionekana kushtushwa sana na jibu yake.

"Unatimiza miaka mingapi?" Ivanna alimuuliza mamake.

Betty Kyallo ambaye alikuwa akirekodi video ya tukio hilo alimjibu binti yake, "Natimiza miaka 34."

Ivanna ambaye wakati huo alikuwa akinywa kitu kutoka kwenye glasi alisema "wueh!" kwa sauti kubwa ya mshtuko.

Kufuatia jibu hilo, mfanyibiashara huyo wa nywele na urembo alimuomba binti huyo wake kwa utani aache kumuaibisha.

"Aah, wewe acha hizo," alisema kabla ya kuangua kicheko.

Betty Kyallo atakuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 34 katikati mwa mwezi ujao. 

Ivanna, ambaye ni mtoto wake na aliyekuwa mume wake, mtangazaji Dennis Okari kwa upande wake atatimiza miaka tisa mwezi Juni mwaka huu.

Betty na Denni Okari walitengana mwaka wa 2016, takriban nusu mwaka tu baada ya kufunga pingu za maisha katika hafla ya harusi ya kifahari. Watangazaji habari hao wawili walikuwa wamechumbiana kwa takriban miaka minne na walikuwa wamebarikiwa kupata mtoto mmoja, Ivanna wakati huo.

Mwaka jana, Betty Kyallo aliweka wazi kwamba hakuna uhasama wowote kati yake na mume huyo wake wa zamani.

Betty alifichua kwamba kuna ushirikiano mzuri kati yake na Okari katika malezi ya binti yao wa Ivanna.

"Kushirikiana katika malezi kumekuwa kuzuri. Ivanna anampenda sana babake na babake vilevile anampenda," Betty alisema akiwa kwenye mahojiano na Citizen Digital.

Mtangazaji huyo mwenye umri wa miaka 33 hivi hata hivyo alikiri kwamba ilichukua muda kabla ya wao kuweza kushirikiana vizuri baada ya ndoa yao kugonga ukuta takriban miaka saba iliyopita.

Alifichua kila mmoja wao huwa anapata muda wa kukaa na binti yao na huwa wanahudhuria mikutano yake shuleni pamoja.

"Huwa tunaenda na Dennis kwenye mikutano yote ya shule. Jinsi huwa tunaketi watu wanaweza kufikiri bado tuko pamoja. Hatuna ugomvi. Sisi ni marafiki. Huwa tunapigiana simu kila wakati kuhusiana na binti yetu," Alisema.

Siku za hivi majuzi, Betty amekuwa akidokeza kwamba tayari yupo kwenye mahusiano mengine ila hajamfichua mpenziwe mpya.