Msamaha? Diamond amnunulia Zuchu pambo la thamani baada ya kudaiwa kumsaliti kimapenzi

Diamond alidaiwa kumcheza Zuchu na mwanamke mwingine nchini Uingereza.

Muhtasari

•Diamond alionekana kwenye video akiwa ameshika cheni maridadi ya fedha yenye kichwa cha malkia ambayo alinunua katika duka moja la mapambo jijini humo.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya bosi huyo wa WCB kuthibitisha kutengana na binti huyo wa Khadija Kopa.

katika ziara yao ya Ufaransa.
Diamond Platnumza na anayedaiwa kuwa mpenziwe, Zuchu katika ziara yao ya Ufaransa.
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Siku chache tu baada ya kuthibitisha kutengana kwao, bosi wa WCB, Diamond Platnumz ameonyesha mapenzi makubwa kwa msanii wake Zuhura Othman almaarufu Zuchu kwa kumnunulia pambo la bei ghali.

Staa huyo wa Bongo ambaye kwa sasa yuko jijini London, Uingereza alionekana kwenye video akiwa ameshika cheni maridadi ya fedha yenye kichwa cha malkia ambayo alinunua katika duka moja la mapambo jijini humo.

Kulingana na taarifa kwenye ukurasa rasmi wa Wasafi, alinunua cheni hiyo inayomeremeta maalum kwa Zuchu.

"Simba amenunulia Zuchu pambo jipya kabisa jijini London," taarifa hiyo ilisoma.

Wimbo wao 'Mtasubiri' ambao unawasuta wanaochukia uhusiano wao uliambatanishwa na video hiyo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya bosi huyo wa WCB kuthibitisha kutengana na binti huyo wa Khadija Kopa.

Katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa Instagram, staa huyo wa Bongofleva aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena.

Diamond alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."

Hapo awali, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yao kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Binti huyo wa Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Diamond aliendelea kuongeza wasiwasi miongoni mwa mashabiki wao huku akichapisha ujumbe wa kimafumbo kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao ulionekana kuzungumzia uhusiano wake.

Mwimbaji huyo alikubaliana na maneno ya meme iliyosomeka, “Muweke mpenzi wako mbele na umuone akianza kukutumia vibaya.

Kwa chapisho hilo, Diamond alionekana kudokeza kuwa Zuchu amekuwa akijinufaisha na yeye kutokana na mapenzi yake makubwa kwake.

Huenda kitendo chake cha kumnunulia cheni malkia huyo wa Zanzibar ni cha kuomba msamaha kwa yaliyotokea.