Karen Nyamu adokeza kuwania ugavana Nairobi, Sonko amshauri amfanye Samidoh naibu wake

"Samidoh akuwe naibu wako ikue kanairo ya Mugithi," Sonko alisema.

Muhtasari

•Karen Nyamu amedokeza kuhusu mpango wake wa kuwania ugavana wa Nairobi katika siku za usoni.
•Sonko alimwambia Nyamu itakapofika wakati wake kuwania, amchukue mzazi mwenzake, Samidoh kama mgombea mwenza.

Mike Sonko, Karen Nyamu, Samidoh
Image: FACEBOOK

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amedokeza kuhusu mpango wake wa kuwania ugavana wa Nairobi katika siku za usoni.

Siku ya Ijumaa, wakili huyo aliyezingirwa na drama si haba alichapisha picha yake akiwa nje ya ofisi ya gavana wa Nairobi na kuambatanisha na ujumbe ulioashiria anatazamia kuchukua wadhifa huo siku moja.

"Kanairo ipo siku! Habari ya asubuhi," aliandika.

Kama kawaida, Wakenya watumizi wa mitandao walijumuika chini ya chapisho hilo kutoa maoni kuhusu taarifa ya mwanasiasa huyo.

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Sonko ni miongoni mwa mamia ya wanamitandao ambao walitoa maoni. Sonko alichukua fursa hiyo kumshauri Bi Nyamu huku akimwambia itakapofika wakati wake kuwania, amchukue mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kama mgombea mwenza.

"Ndio, na Samidoh akuwe naibu wako ikue kanairo ya Mugithi," alimwambia.

Nyamu hata hivyo hakujibu ujumbe wa gavana huyo wa zamani. Baadhi ya wafuasi wake wengine pia walimtia moyo kupigania nafasi hiyo ya uongozi siku za usoni huku wengine wakimkatiza tamaa.

Takriban miezi mitano iliyopita, Sonko alifichua kwamba yeye ndiye aliyemuunganisha Samidoh na seneta huyo wa kuteuliwa.

Gavana huyo wa zamani alidai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita. Sonko alikuwa akitoa maoni chini ya chapisho  la Nyamu kwenye Facebook wakati alipotoa ufichuzi huo.

"Mnafaa mniitie chai. Mimi ndio nilikupea Samidoh pale Dubai nikiwa na Moses Kuria wakati wa Mugithi night," alimwambia Karen.

Karen ambaye kwa sasa ana watoto wawili pamoja na Samidoh hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," alimjibu Sonko.

Sonko anaonekana kuwa na uhusiano wa karibu sana na wazazi wenza hao wawili na mara kadhaa amekuwa akionekana nao. Nyamu alianza kuchumbiana na mwimbaji huyo wa Mugithi miaka michache iliyopita na wamekuwa katika uhusiano wenye utata ambao umepelekea kuzaliwa kwa watoto wawili.