Mwimbaji aliyeshirikiana na Diamond, Mbosso afariki akitumbuiza jukwaani, wamwomboleza kwa uchungu (+video)

Costa Titch alizirai ghafla akiwa jukwaani na baadaye kutangazwa amefariki.

Muhtasari

Costa Titch alikuwa akitumbuiza katika tamasha la Ultra Music wakati alipozimia ghafla  na baadaye kutangazwa amekata roho.

โ€ขDiamond na Mbosso, waliwahi kufanya kazi na Costa wamemwomboleza na kuonekana kuvunjwa moyo sana na kifo chake.

Marehemu Costa Titch na Mbosso
Image: INSTAGRAM// MBOSSO

Mwimbaji mashuhuri wa Afrika Kusini, Costa Tsobanoglou, almaarufu Costa Titch ameripotiwa kufariki baada ya kuzirai jukwaani.

Costa Titch alikuwa akitumbuiza katika tamasha la Ultra  Music lililofanyika Expo Centre jijini Johannesburg  usiku wa Jumamosi, 12 Machi 2023 wakati alipozimia ghafla akiwa  jukwaani na baadaye kutangazwa amekata roho.

Mwimbaji huyo ambaye pia ni mcheza densi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 27. Alizaliwa na kukulia Nelspruit, Mpumalanga.

Marehemu anajulikana kwa nyimbo zake maarufu kama Nkalakatha, Big Flexa na Activate. Pia aliwahi kushirikiana na staa wa Bongo Diamond Platnumz kwenye kibao Superstar na Mbosso kwenye kibao Shetani na Moyo.

Waimbaji hao wa WCB ambao waliwahi kufanya kazi na Costa wamemwomboleza na kuonekana kuvunjwa moyo sana na kifo chake.

"Dah๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ" Diamond aliandika chini ya picha ya mwimbaji huyo ambayo alichapisha kwenye Instagram.

Mbosso kwa upande wake alichapisha picha yake ya kumbukumbu na Costa Titch na chini yake kuonyesha jinsi alivyositikishwa.

"Costaaaa๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ˜ญ๐Ÿ’”," aliandika.

Pia alipakia video ya mwaka wa 2022 inayoonyesha akicheza densi na marehemu wakiwa ndani ya nyumba.

Kifo cha Costa Titch kimekuja wakati mashabiki wa muziki wa Afrika Kusini wakiwa bado wanaendelea kumuomboleza  mwimbaji mwenzake, rapa AKA, ambaye jina lake halisi ni Kiernan Forbes.

AKA alipigwa risasi nje ya mgahawa jijini Durban na watu wasiojulikana. Polisi wa Afrika Kusini (SAPS) bado wanachunguza kesi hiyo. Cha kushangaza ni kwamba, Costa Titch na AKA wameshirikiana kwenye wimbo unaoitwa Super Soft.