Esther Musila, mke wa mwanamuziki wa injili Guardian Angel amefichua kwamba chuki ya watu mitandaoni dhidi yake wala haikoseshi usingizi hata kidogo kwenye maisha yake. Chuki na kejeli mitandaoni pia alisema hazijawahi zua mkwamo wowote katika ndoa yake na msanii Guardian Angel.
Musila aliweka wazi kwamba wale wote wanaoendeleza chuki na kejeli dhidi yake wanafanya kazi bure kwani hawamkomoi hata chembe.
Mama huyo wa watoto watatu alisema kwamba katika maisha yake, hana nguvu wala uwezo hata kidogo kwenye nafsi yake kulipiza chuki kwa chuki, na hio halijawahi muingia akilini hata kidogo.
Dawa ya wenye chuki kulingana na Musila, ni kuwapenda, kuwatakia mema au kuwaombea wapone kutokana na chuki hiyo.
“Sina nguvu hata kidogo nafsini mwangu kumchukia mtu yeyote. Kiuhalisia sina nafasi hiyo katika moyo wangu. Ukinichukia ni ama nikuombee upone, nikupende au nikutakie mema,” Musila alisema.
Musila na mumewe Guardian Angel wamekuwa wakikejeliwa mitandaoni kwa ndoa yao kutokana na utofauti mkubwa uliopo baina ya umri wao.
Musila amemuacha Angel kwa takribani miaka 20 na hilo limekuwa likiibuliwa kama gumzo la kigezo cha umri katika ndoa baina ya mume na mke kila mara, Zaidi ya mwaka mmoja tangu wawili hao kuwa mwili mmoja katika hafla ya faraghani.
Wikendi iliyopita, Musila alifichua kwamba licha ya watu wengi kumshambulia hadharani kutokana na umri wake mkubwa, lakini mamia ya watu hao hao ndio aghalabu hufurika kwenye faragha za kurasa zake mitandaoni wakitupa ndoana kwa moyo wake.