Mwanasoshalaiti maarufu wa Uganda Zari Hassan na mpenzi wake mdogo Shakib Cham Lutaaya wameendelea kufurahia mahusiano yao na kuwazima wakosoaji wao.
Siku ya Jumapili, mzazi mwenza huyo wa staa wa bongo Diamond Platnumz alichapisha picha nzuri zilizomuonyesha yeye na Shakib wakiwa likizoni huko Dubai, UAE.
"Katikati ya mahali💕," aliandika chini ya picha hizo ambazo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Pichani, wapenzi hao ambao walivalia nguo nyeusi na vitambaa vya Kisomali walionekana wenye furaha tele huku wakikumbatiana kimahaba. Baadhi ya picha ziliwaonyesha kwenye gari ndogo la jangwani.
Wawili hao hata hivyo hawaweka wazi ni lini walienda likizo hiyo ya jangwani na kwa muda gani wangekuwa kule.
Wiki jana, Shakib alimsherehekea mama huyo wa watoto watano kwa ujumbe maalum mnamo siku ya kuadhimisha wanawake duniani.
Shakib, 31, alimtambua mpenzi huyo wake kwa jukumu lake la kuwatia moyo watu wengine na kumtaka kuendelea.
"Heri ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwako Mpenzi! Wewe ni msukumo kwa wengi, endelea na kazi nzuri," alimwandikia mpenziwe.
Shakib aliandika ujumbe huo mzuri chini ya chapisho la Zari akiwatakia wanawake wote duniani siku njema ya wanawake.
Zari alipenda ujumbe wa mpenzi huyo wake mdogo na akachukua fursa kumshukuru.
"Asante boo," alijibu.
Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz amekuwa kwenye mahusiano na Shakib Lutaaya kwa miezi kadhaa sasa na wawili hao wamekuwa wakionyesha wazi jinsi wanavyofurahia kuwa pamoja.
Wawili hao walianza kuchumbiana katikati ya mwaka jana na uhusiano wao umekabiliwa na ukosoaji mwingi haswa kutokana na tofauti zao kubwa za umri. Zari ana miaka 42 huku Shakib akiwa mdogo kwa miaka 10 kuliko yeye.