Fahamu kisa cha mvulana aliyerekodiwa akilia kisha kucheka ghafla kwenye video maarufu

Albert alianza kulia baada ya mamake kukosa kumpikia chakula alichokuwa akitaka.

Muhtasari

•Video ya Albert Ofusu Nketia, 7, imekuwa ikivuma sana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kutumiwa kama meme.

•Mamake Albert alifichua kuwa mwanawe alizaliwa akiwa na hali maalum.

Albert Ofusu Nketia
Image: HISANI

Familia ya mvulana ambaye alirekodiwa akilia na mara moja akabadilika na kuanza kucheka hatimaye imevunja kimya kuhusu kile kilichotokea.

Video ya Albert Ofusu Nketia, 7, imekuwa ikivuma sana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kutumiwa kama meme katika siku za hivi majuzi.

Kwenye mahojiano na Oheneba Media, mamake Albert, Rosina alifichua kwamba mwanawe alikuwa akilia kwa sababu alitaka kula viazi vikuu lakini kwa bahati mbaya hakukuwa navyo nyumbani. Katika jitihada za kumtuliza, nyanyake alianza kumuimbia wimbo wa kuchekesha ambao ulimfanya aangue kicheko.

Ilikuwa ni siku ya Jumamosi akasema anataka kula viazi vikuu, mimi nilikuwa nafua nguo wakati huo na sikuwa nazo nyumbani. Sikujua nichukue hatua  niende sokoni ili ninunue ama vipi," alisimulia.

Kufuatia hayo, Bi Rosina aliamua kumpikia mwanawe chakula mbadala, jambo ambalo halikumpendeza.

"Nilikuwa na ndizi mbichi wakati huo hivyo nikampikia. Alipoona kitoweo hicho na kutafakari jinsi kingeendanisha vizuri na viazi vikuu vya kuchemsha kuliko ndizi, alianza kulia," mamake Albert alisimulia.

Bi Rosina na nyanyake Albert walijaribu kumshawishi akule ndizi na akakubali. Alikula mpaka ikabaki chakula kidogo tu.

"Nyanya yake alimuuliza “kwahiyo umekula ndizi hii?” kisha akaanza kulia tena, katika jitihada za kumfanya aache kulia,  nyanyake alianza kumwimbia wimbo wa kipekee kisha kicheko kikaanza katika harakati hizo hadi kikaisha," alisema.

Rosina alisema video hiyo haikukusudiwa kutoka nje ya boma na ilisambaa baada ya simu iliyotumika kurekodi kuuzwa na mtu mwingine kuipakia mtandaoni. Alisema hakupenda jambo hilo na hata alimkasirikia aliyehusika. 

“Nilipokutana na mwanaume huyo baada ya kunisalimia, hata sikumjibu kwa sababu nilihisi alifaa kunieleza kwanza,” alisema.

Mamake Albert pia alifichua kuwa mwanawe alizaliwa akiwa na hali maalum lakini anaendelea kumfunza aishi maisha ya kawaida.