Vanessa Mdee atazamia kurejea tena kwenye tasnia ya muziki

"Namuamini Mungu kwa hatua yangu inayofuata kama mtumbuizaji. Nasubiri maagizo yake," alisema

Muhtasari

•"Namuamini Mungu kwa hatua yangu inayofuata kama mtumbuizaji. Nasubiri maagizo yake," alisema.

•Mwaka wa 2020, Mdee aliwafanya mashabiki kuamini kuwa ameacha muziki.

Vanessa Mdee na Rotimi
Image: Vanessa Mdee Instagram

Mwimbaji wa Tanzania Vanessa Mdee amedokeza kurejea kwake tena kimuziki.

Mdee alichapisha video ya kumbukumbu alipokuwa akitumbuiza kwenye Jukwaa la Crans Montana mwaka wa 2019.

"Namiss kutumbuiza," aliandika.

"Namuamini Mungu kwa hatua yangu inayofuata kama mtumbuizaji. Nasubiri maagizo yake."

Mwaka wa 2020, Mdee aliwafanya mashabiki kuamini kuwa ameacha muziki. Akizungumza kwenye podcast yake, aliitaja tasnia ya muziki kama ya pepo.

"Nilihitaji kuchagua maisha yangu, tasnia ya muziki ni ya kishetani," Vanessa alisema kwenye podikasti.

"Sasa mashabiki wangu labda wanajiuliza hivi sasa, 'Je, hautaimba tena? Je, hatutakuona ukitumbuiza?' Acha nirudie tena. Ninapenda muziki, napenda kuunda, na napenda kutumbuiza. Ninaimba. Mimi ni chombo."