Esther Musila afichua alivyonufaika na ndoa yake na Guardian Angel

"Nilikuchagua na nitakuchagua tena na tena," Musila alimwambia mumewe.

Muhtasari

•Musila alimsherehekea mwimbaji huyo na kumhakikishia kwamba yeye ndiye mwenzi wa maisha wa chaguo lake.

•Mama huyo wa watoto watatu alikiri kuwa hakupata tu mume katika Guardian Angel, bali pia rafiki yake wa kweli.

Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Bi Esther Musila, kwa mara nyingine amekiri mapenzi yake yasiyoisha kwa mume wake Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel.

Siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alimsherehekea mwimbaji huyo wa nyimbo za injili na kumhakikishia kwamba yeye ndiye mwenzi wa maisha wa chaguo lake.

"Nilikuchagua na nitakuchagua tena na tena," Musila alimwambia mumewe kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alikiri kuwa hakupata tu mume katika Guardian Angel, bali pia rafiki yake wa kweli.

"Bila kusita bila shaka, kwa mpigo wa moyo, nitaendelea kukuchagua. Ndani yako nilipata upendo wa maisha yangu, na rafiki yangu wa karibu zaidi," alisema.

Guardian Angel alijibu ujumbe wa mkewe kwa kuthibitisha mapenzi yake makubwa kwake.

Siku ya Jumanne, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alimsherehekea mke huyo wake kwa kuchapisha video yake akitoka nyumbani.

"Habari za mchana mpenzi wangu,” Musila alijibu chini ya video hiyo.

Mwezi uliopita, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alifichua kwamba aliombea muungano wake na Guardian Angel.

Akizungumza kwenye video, alifichua kuwa takriban miaka minne iliyopita, aliomba  kumsihi Mungu abadilishe maisha yake.

"Niliomba kwamba wakati nitafikisha miaka 50 mwaka wa 2020, Mungu abadilishe maisha yangu kabisa," Bi Musila alisema.

Mhasibu huyo alisema aliendelea kusali na kumwomba Mungu ampatie maana katika maisha yake. Alidokeza kuwa Mungu alijibu maombi miezi michache baadaye kwa kumletea mumewe Guardian Angel maishani.

“Mume wangu Peter Omwaka, namshukuru Mungu kwa ajili yako, namshukuru Mungu kwa kukuleta katika maisha yangu, kwa kukutumia kubadilisha maisha yangu, kwa kunionyesha upendo na unyenyekevu na kuyafanya maisha yangu kuwa mazuri,” alisema.

Musila alisema hayo akiadhimisha miaka mitatu tangu alipokutana na Guardian Angel siku ya Jumatatu, Machi 13, 2023.  Alisema tarehe 13 mwezi Machi daima itasalia kuwa maalum na ya maana kwake.

Wakati huo, Guardian Angel kwa upande aliweka wazi kuwa alimpenda mkewe punde baada ya kukutana naye. Katika taarifa yake, Angel alisema alipomwangalia Bi Musila aliona sifa zote anazohitaji kwa mke ndani yake.

"13/3/2020 ulinitazama ukaona supastaa. Hamu yako ilikuwa kuniona nikiwa vile ulivyoniona. Nilikutazama na kuona kila nilichotaka kwa mwanamke. Miaka mitatu baadaye sisi sote tuna kile tulichotaka," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alimtaja Bi Musila kuwa mke mzuri na kukiri mapenzi makubwa kwake.