Kwa siku ya pili sasa msanii Nandy amekuwa akipigana vita na media ya Wasafi inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kisa mtangazaji mmoja kusema kwamba Nandy amepoteza ushawishi na umaarufu tangu alipoingia kwenye ndoa na Billnass mwaka mmoja uliopita.
Mtangazaji wa kipindi cha asubuhi katika redio ya Wasafi alitoa kauli kwamba Nandy hawezi hata kumshawishi binti yake kwa njia yoyote, akiibua dhana kwamab msanii wa kike anapoingia kwenye ndoa ushawishi wake huporomoka.
“Kitendo cha Nandy kuolewa na kupata mtoto kunaweza kumpunguzia ushawishi kwa vijana. Watumizi wakubwa wa muziki ni vijana, sasa pale msanii anapotangaza kuingia katika ndoa, ana asilimia kubwa za kupunguza ushabiki. Mfano mzuri ni Nandy,” mtangazaji huyo alinukuliwa.
Hata hivyo, maneno haya ya kumkandia Nandy hayakupokelewa vizuri naye na alijibu kwa kughadhabishwa akisema kuwa hata kama wameshindwa kuficha chuki basi wanafaa kukubali kile kidogo ambacho anakifanya.
“Heshimuni basi hata kidogo ninachokifanya kama mmeshindwa kuficha chuki zenu,” Nandy alijibu akimalizia kwa emoji za kulia na kuvunjika moyo.
“Nimekaa muda mrefu sana nikiamini maneno yenu na chuki za wasiwasi haziwezi kuondoa kile ambacho Mwenyezi Mungu amepandikiza ndani yangu. Lakini sasa hili limezidi, wacha niseme. Mimi ni binti na sasa ni mama na kwa muda mrefu nimekuwa nikipambania ndoto zangu kwa jitihada zangu mwenyewe ili kusaidia familia yangu…..” Nandy alitema lalamiko refu.
Nandy alisema kuwa si mara ya kwanza media ya Wasafi kuandika maudhui hasi kumhusu, akisema kuwa ni mwaka wa tatu sasa wamekuwa wakijaribu kumuangusha bila kujali kwamba ana watu wengi wanaomtegemea, kutoka familia hadi vijana wenzake ambao amewaajiri.
“Kila siku mmekua mkiandika mambo hasi kuhusu mimi na huku nyuma mmekuwa mkituma watu kuniomba mahojiano ambayo nilikataa sababu najua mna nia kandamizi juu ya biashara yangu. Nimekuwa nikifanya vitu vizuri lakini hamjawahi kuandika wala kuvipa kipaumbele,” Nandy aliendelea kulalamika.
Baadhi walihisi kwamba Wasafi wameanza kumchafua Nandy kama ambavyo walijaribu kumchafua Harmonize kwa mara kadhaa baada ya kuondoka Wasafi, nia yao kubwa ikiwa kumuona anahangaika na kutokomea kabisa.