Mbunge wa Mumias East Peter Salasya amekuwa mtu wa hivi punde kiweka kwenye mizani suala la kukamatwa kwa mchungaji wa kanisa la New Life Prayer Center huko Mavueni kaunti ya Kilifi, Ezekiel Odero.
Odero alitiwa mbaroni jana kwa kuhusishwa na mchungaji mwingine mwenye utata Paul Mackenzie ambaye shamba lake la ekari 800 limetangazwa rasmi na serikali kuwa makaburi ya jumla huko Shakahola.
Mpaka sasa, DCI wamefukua miili Zaidi ya 100 ya watu wanaoaminika kuwa ni waumini wa Mackenzie ambao walifariki wakiwa wanajitesa njaa ili ‘kumuona Yesu’
Kukamatwa kwa Odero ni kufuatia kile ambacho DCI walitaja kuwa wana tarifa za kijasusi ambazo zinamhusisha na Mackenzie, wakisema kuwa baadhi ya watu ambao walifariki karika kanisa lake walisafirishwa kwa lori kwenda Shakahola kwa shamba la Mackenzie kwa ajili ya maziko.
Hata hivyo, Salasya amemtetea vikali Odero alizitaka idara zote kufanya uchunguzi wao dhidi ya Mackenzie pasi na kumuingiza Odero kwenye sakata hilo.
“Mchungaji Ezekiel anapaswa kuachwa mbali na matatizo yanayoletwa na Mackenzie. Polisi, DCI, mwendesha mashitaka, EACC, mahakama n.k walipata fursa ya kuwalinda wananchi waliopotoshwa kifikira lakini badala yake walinyamaza .Hakuna anayepaswa kumvamia mchungaji Ezekiel, kama amepata kituo, tatizo nini?” aliuliza Salasya.
Alhamisi baada ya Odero kukamatwa, mbunge wa Magarini Harrison Kombe alikuwa mtu wa kwanza kumtetea mwinjilisti huyo akisema kuwa anaamini katika miujiza yake kwani kwa kipindi kimoja aliwahi kufika katika kanisa lake na kusujudu.
“Kuna watu wametoka katika eneo bunge langu na kwenda mpaka kanisa la Ezekiel kwa ajili ya maombi na kurudi wakiwa katika hali salama. Na pia kwa ufahamu, ni kwamba sasa hivi Ezekiel anajenga chuo cha madaktari katika eneo lake,” Kombe alisema.
“Kwa sasa naweza sema mambo yake ni halali kwa sababu nimeshuhudia, nimewahi hata kufika kanisani na kusujudu pale. Na kama ni miujiza kufanyika inafanyika hapo hapo unaona, si mambo ya kwamba inakwenda kufanyiwa gizani halafu unaletewa huyo mtu, hapana,” mbunge Kombe alisema.
Kombe alikiri kwamba endapo atafunguliwa mashtaka ya kutoa mafunzo ya kupotosha, binafsi atashangaa sana.