"Itanila maisha yangu yote!" Bintiye Kajala, Paula ahuzunika kwa kuhusishwa kimapenzi na Harmonize

'"Unadhani watoto wenzangu wananichukulia vipi kwamba mimi nimeshare mwanaume na mama yangu?"-Paula

Muhtasari

•Kajala alifunguka jinsi Paula alivyodaiwa kushiriki mahusiano ya kimapenzi na Harmonize wakati akichumbiana naye.

•Kajala alieleza kuwa Paula alihofia kuwa madai ya marafiki zake kuhusu uhusiano wao na Harmonize zingemfuata daima.

Image: INSTAGRAM// PAULA KAJALA

Muigizaji Fridah Kajala Masanja na binti yake Paula Paul wameendelea kufichua mengi kuhusu maisha yao katika filamu ya maisha halisi 'Behind The Gram' ambayo inaendelea kupeperushwa kwenye Zamaradi TV.

Katika kipindi cha hivi majuzi, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alifunguka kuhusu jinsi binti yake alivyodaiwa kushiriki mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji huyo wa bongofleva wakati akichumbiana naye.

Alisema kuwa bintiye alisononeka sana baada ya marafiki zake kumhusisha na bosi huyo wa Konde Music Worldwide.

"(Paula) Anaweza kuwa amesema nimekusamehe kwa sababu mimi ni mamake ananipenda lakini sijui moyo uko vipi," Kajala alifunguka wakati akizungumza na mwanaume aliyeonekana kuwa mwanasaikolojia.

Alieleza kuwa Paula alihofia kuwa madai ya marafiki zake kuhusu uhusiano wao na Harmonize zingemfuata daima.

"Kuna siku ashawahi kunitamkia akaniambia 'unadhani mimi watoto wenzangu wananichukulia vipi kwamba mimi nimeshare mwanaume na mama yangu?" Akaendelea kusema hii itanila maisha yangu yote," alisimulia.

Kajala alidokeza kwamba wakati mwingine binti huyo wake mwenye umri wa miaka 20 hufichua maumivu makubwa aliyo nayo ndani yake kuhusu jambo hilo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Mwako wa 2021, mugizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alitengana na Konde Boy kwa mara ya kwanza baada ya kuchumbiana kwa miezi michache. Kulikuwa na madai kwamba alimtema mwimbaji huyo kwa kujaribu kumtongoza Paula.

Wawili hao hata hivyo walirudiana mwezi Mei mwaka jana baada ya bosi huyo wa Konde Gang kuomba msamaha. Walitengana kwa mara ya pili mwezi Desemba licha ya awali kuonyesha mahaba mazito kati yao.

Hivi majuzi Kajala akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha hapa nchini, alidokeza kuwa alimtema mwimbaji huyo kwa sababu ya mazoea.

"Sijui niseme nini. Labda mazoea. Mtu akishakuzoea sana anakuchukulia poa," alisema.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alidokeza kwamba Harmonize bado hakuwa tayari wakati alipoamua kutulia naye kwenye mahusiano na kuwa huenda alihitaji nafasi ya kufanya mambo yake binafsi.

"Yaani mimi hata simlaumu, kwa sababu yeye ni kijana mdogo. Labda alihitaji nafasi, tulikuwa tuko karibu sana.

Yeye mara ya kwanza nahisi labda aliona kama mzaha akisema nataka huyu mtu, nataka niwe naye 24/7.  Mnaamka wote mnaenda gym, mnafanya hiki na kile. Labda alikuwa anahitaji nafasi yake afanye vitu vyake," alisema.

Kajala alibainisha kwamba alikubali kurudaina na bosi huyo wa Konde Music Worldwide kwa kuwa bado alikuwa anampenda.