Gidi alalamikia Young,Famous and African; aeleza kwa nini Akothee anafaa kushirikishwa

Gidi alibainisha kwamba filamu halisi ya Kiafrika ni sharti iwe na wahusika wachawi na madaktari wa kienyeji.

Muhtasari

•Gidi ameibua wasiwasi kuhusu kipindi maarufu cha maisha halisia cha Young, Famous and African kwenye mtandao wa Netflix.

•Licha ya kulalamika, mtangazaji huyo hata hivyo alisifu utayarishaji wa filamu hiyo akisema ni wa ubora wa hali ya juu.

Mtangazaji Gidi Ogidi na Akothee
Image: INSTAGRAM//

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi ameibua wasiwasi kuhusu kipindi maarufu cha maisha halisia cha Young, Famous and African kwenye mtandao wa Netflix.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, mtangazaji huyo mahiri alilalamika kwamba filamu hiyo imeiga sana mtindo wa Marekani.

Gidi alidokeza kwamba angekuwa mtayarishaji wa filamu hiyo angehakikisha kuna wahusika wenye tabia za kawaida vya Kiafrika akitoa mfano wa mwanamuziki na mjasiriamali wa Kenya, Esther Akoth almaarufu Akothee.

"Kama ningekuwa mtayarishaji, ningemwalika Akothee wetu akuje na kapanga hako kake ambako huwa anatumia kufyeka vichaka na njia huku akilalamika kuhusu masuala mbalimbali," Gidi alisema kwenye Facebook.

Alidokeza kuwa ingekuwa yeye ndiye mtayarishaji angehakikisha kuna kipindi ambapo mama huyo wa watoto watano anawakimbiza wahusika wengine kwenye shoo hiyo na panga hadi waache lafudhi yao bandia.

"Halafu juju man kutoka Nigeria atokee na kumgeuza kuwa  chungu kisha kumrudisha Kenya. Sasa hiyo ndiyo drama halisi ya Kiafrika,"

Gidi alibainisha kwamba filamu halisia ya Kiafrika ni sharti iwe na wahusika wachawi na madaktari wa kienyeji.

"Na kwa nini wanasukuma wazo lao la mwanamke kuzaliwa mtoto na mwanamke mwingine na maneno ya LGBTQ?" alihoji.

Licha ya kulalamika, mtangazaji huyo hata hivyo alisifu utayarishaji wa filamu hiyo akisema ni wa ubora wa hali ya juu.

Haya yanajiri baada ya mwanamuziki Akothee kuthibitisha kwamba amekuwa akifuatilia kipindi hicho cha Netflix ambacho kimewaleta pamoja mastaa mashuhuri kutoka mataifa tofauti ya Afrika.

Hivi majuzi, alitoa maoni yake kuhusu sehemu ya pili ya filamu hiyo iliyoachiwa hivi majuzi ambapo alimsifu mwanamitindo maarufu wa Nigeria Swanky Jerry kuhusu mitindo na ucheshi wake uliomvutia.

"Swanky. Usumbufu wa Young Famous African. @swankyjerry ndiye shoo yenyewe, huyu jamaa ananichekesha. Wakati anaingia, mazingira yanabadilika. Swanky ni yule Rafiki mmoja kwenye kikundi ambaye hutajua lini na jinsi ya kumzungumzia… Hisia zake za mitindo ! Ucheshi unahitaji kiwango fulani cha akili," Akothee alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alionekana kumtetea aliyekuwa rafikiye, Zari Hassan kuhusu ugomvi wake na Fantana.

"Fantana ni msichana mdogo asiye na heshima ambaye anahitaji kukua. Huwezi kushinda vita ya baby mama. Sikupenda, hakuna kiboko hapo." alisema.